Na: Gladness Mphuru
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo
(SUA) kimesaini Mkataba wa Ushirikiano na Taasisi 7 za Wizara ya Kilimo wenye lengo
la kukuza uchumi wa Nchi kupitia Sekta ya Kilimo.
Zoezi hilo limefanyika Februari
9, 2023 katika Kampasi ya Edward Moringe Sokoine mkoani Morogoro ambapo
limeongozwa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu
Prof. Maulid Mwatawala kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo cha SUA, Prof. Raphael
Chibunda.
Prof. Mwatawala amesema wamepata
mafanikio makubwa kwa sababu mwanzo SUA ilikuwa na mashirikiano na Taasisi moja
ya Wizara ya Kilimo ambayo ni Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kisha zikaongezeka na kuwa nne(4) ambazo ni
TARI, Wakala wa Mbegu Tanzania (ASA) na Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) na kisha Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), Mamlaka inayoshughulikia Udhibiti wa Mbolea (TFRA),
na Mamlaka ya Afya ya Mimea na Udhibiti wa Viuatilifu) TPHPA.
Amesema kufuatia agizo la Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe wakati wa ziara na Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo chuoni hapo Mkataba huo pia imewajumuisha Vituo vya Mafunzo ya Kilimo (MATI).
“Makubaliano yatatuweka karibu ili
kutimiza majukumu kwa pamoja lakini pia hayana lengo la kukwamisha jukumu la
mtu yeyote tunachosaidiana ni kuisaidia Wizara ya Kilimo katika utekelezaji wa
majukumu yake” amesema Prof. Mwatawala.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu TOSCI,
Stanford Chijenga Amesema karibu asilimia 90 ya wafanyakazi wao ni wahitimu wa
SUA na kila mwaka wanatenga kiasi cha million 70 kwa ajili ya kuwasomesha
wanafunzi na zimekuwa zikienda SUA.
Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mbegu Dkt.
Sophia Kashenge amesema ushirikiano huu una manufaa makubwa kwao kwa sababu
hapo nyuma walikuwa wanafanya kazi kwa pamoja bila makubaliano lakini sasa
watafanya kazi na Taasisi hizo kwa umoja na pia wanapokea wanafunzi kutoka SUA
jambo ambalo litaongeza wigo mpana wa kufanya kazi.
“Sisi kama wazalishaji wa Mbegu kuna maeneo
tulikuwa tunaona tungefanya kazi vizuri tunaamini SUA wana mbegu nyingi ambazo
wamezitoa na bado hazijafika kwa wakulima kwa hiyo kwa ushirikiano huu
tunaamini tunaweza kuzalisha mbegu kwa pamoja” amesema Dkt. Kashenge
Taasisi ambazo zimeingia makubaliano ni SUA, TARI, ASA, TOSCI, NIRC, TFRA, TPHPA na MATI.
0 Comments