SUAMEDIA

Maafisa Mawasiliano watakiwa kufikisha Taarifa sahihi kwa wakati kuepusha Upotoshaji

 Na: Farida Mkongwe

Maafisa Mawasiliano waliopo Serikalini wametakiwa kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuwa na Mawasiliano ya Kimkakati yatakayowawezesha kufikisha taarifa sahihi kwa wananchi kuhusu juhudi zinazofanywa na Serikali katika kukabiliana na changamoto mbalimbali.

 Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa akiwasilisha mada kuhusu Mawasiliano ya kimkakati katika mkutano 107 wa Washitiri wa vipindi vya Elimu kwa Umma mkutano unaendelea mkoani Morogoro

Wito huo umetolewa Februari 20, 2023 na Msemaji Mkuu wa Serikali ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Gerson Msigwa wakati akitoa Mada kuhusu Mawasiliano ya Kimkakati wakati wa Mkutano wa 107 wa Washitiri wa Vipindi vya Elimu kwa Umma unaofanyika mjini Morogoro.

Msigwa amesema ili kuepukana na upotoshwaji unaofanywa na baadhi ya watu wasiokuwa na mapenzi mema na Serikali, Maafisa Mawasiliano hawana budi kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele kuifikishia jamii kazi mbalimbali zinazofanywa na Serikali ikiwa ni pamoja na kuitumia mitandao ya kijamii ambayo imekuwa ikitumiwa na wengi.

“Sasa hivi tuna uhitaji mkubwa wa Mawasiliano ya Kimkakati kuliko wakati mwingine wowote kwa sababu idadi ya watu imeongezeka, baadhi ya maeneo ya kimkakati ni pamoja na kuboresha huduma za kijamii likiwemo suala la Maji, Elimu, Afya, Miundombinu, Madini na Utalii, hivyo tufanye kazi zetu kikamilifu tusipofanya hivyo wachache watachafua taswira ya Serikali”, amesema Mkurugenzi huyo.

Akizungumza katika Mkutano huo Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Habari la Utangazaji Tanzania (TBC) Dkt. Ayoub Rioba amesema Mkutano huo ni wa muhimu sana kwa Washitiri wa Vipindi vya Elimu kwa Umma kwa  kuwa wanapata nafasi ya kujifunza kulingana na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia.

“Washitiri wanafanya kazi muhimu Serikalini na kwingineko ya kuwafahamisha wananchi nini kinaendelea nchini, katika utandawazi tulionao kumekuwa na mabadiliko ya Sayansi na teknolojia hivyo hata vipindi unavyoandaa inatakiwa ujue ulimwengu unahitaji kitu gani”, amesema Dkt. Rioba.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Radio TBC ambaye pia ni Mratibu wa Mkutano huo Bi. Aisha Dachi amesema Mkutano huo uliokutanisha Maafisa Habari na Maafisa Mahusiano zaidi ya 100 umelenga kuwakutanisha pamoja Maafisa hao ili kujenga mahusiano na kubadilishana uzoefu wa namna bora ya kuandaa Vipindi vya Elimu kwa Umma.

Mkutano huo wa siku tano ulioandaliwa na TBC umebeba Kauli Mbiu isemayo “Vyombo vya Habari ni Chachu ya Miradi ya Maendeleo”.


KATIKA PICHA

Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji nchini (TBC), Dkt. Ayub Rioba akizungumza katika katika mkutano 107 wa Washitiri wa vipindi vya Elimu kwa Umma mkutano unaendelea mkoani Morogoro



Baadhi ya Washiriki katika mkutano 107 wa Washitiri wa vipindi vya Elimu kwa Umma wakifuatilia kwa umakini mkutano unaendelea mkoani Morogoro



Post a Comment

0 Comments