SUAMEDIA

Serikali yapongezwa kwa kutekeleza Miradi ya Kimkakati

Na: Farida Mkongwe

Maafisa Habari na Mawasiliano kutoka Wizara na Taasisi mbalimbali za Umma wameipongeza Serikali kwa kuendelea kufanikisha Miradi mikubwa ya Kimkakati ambayo ni chachu ya Maendeleo ndani na nje ya nchi.

Maafisa hao wametoa pongezi hizo Februari 22, 2023 wakati wa ziara yao ya mafunzo ya kutembelea Mradi mkubwa wa Kimkakati wa Reli ya Kisasa (SGR) kwa kipande cha Morogoro hadi Kilosa kwa lengo la kujionea juhudi zinazofanywa na Serikali katika mradi huo na baadaye kutoa taarifa sahihi kwa wananchi. 

“Tumeona majengo mazuri yamefanyiwa ubunifu vizuri, kuna mifumo ya kiusalama na miundombinu ya kisayansi na teknolojia, usafiri huu utakapoanza kutumika utawakwamua watanzania kwa kiasi kikubwa, kwa kweli tunaipongeza Serikali na TBC kwa kuandaa ziara hii ya Mafunzo”, amesema Bw. Fredrick Kalinga Kaimu Meneja Mawasiliano na Masoko kutoka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).

“Tumeiona stesheni ya Morogoro jinsi ilivyokuwa bora na kujitosheleza kwa kila kitu na pia tumekiona kituo cha kupoozea umeme, tumetembelea chumba cha kuongozea treni na sehemu nyingine nyingi na tumeambiwa ujenzi huu kwa kipande cha kwanza umekamilika kwa asilimia 97 tunampongeza Rais Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayofanya, amesema Mshitiri Mariam Hamisi kutoka Dar es Salaam.

Wakiwa wilayani Kilosa Maafisa hao wametembelea handaki refu kuliko yote yaliyopo kwenye njia hiyo ya Reli ya kisasa lenye urefu wa km. 1.031 ambapo Mhandisi Oliva Kinyieni Kaimu Meneja wa Mradi kipande cha pili cha ujenzi wa Reli hiyo ya Kisasa kutoka Morogoro- Makutupora amesema handaki hilo litazuia athari za reli kusombwa na maji yanayotoka katika mto Mkondoa.

Akizungumza katika ziara hiyo Afisa Uhusiano wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Bi. Jamila Abdallah amesema SGR ni Reli ya Kisasa na ya kwanza Afrika Mashariki na Kati itakayokuwa na uwezo wa kupitisha Treni zitakazoendeshwa kwa nishati ya umeme na yenye mwendokasi usiopungua kilometa 160 kwa saa kwa treni za abiria na Kilometa 120 kwa saa kwa treni za mizigo. 










Post a Comment

0 Comments