Na; Ayoub Mwigune
Katika kuhakikisha changamoto ya Wahitimu wa Elimu ya Juu kukosa uzoefu inapatiwa ufumbuzi, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) kimechukua hatua ya kuzikutanisha pamoja Sekta binafsi, Viwanda, Makampuni, na Taasisi zinazotoa mafunzo ya Kitaaluma ili kupanga mikakati ya pamoja ya kuondokana na tatizo hilo.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uzamili, Utafiti, Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalam Prof. Esron Karimuribo jijini Dar es Salaam Januari 17, 2023 wakati akizungumza katika kikao kilichowakutanisha pamoja wadau hao ili kuona namna bora ya kutatua changamoto ya ukosefu wa uzoefu kwa Wahitimu.
Awali Prof. Karimuribo alisema mara nyingi kumekuwa na lawama kati ya Taasisi za Elimu pamoja na Viwanda ambapo Taasisi za Elimu zenyewe zimekuwa zikiamini zinazalisha Wanafunzi bora wenye ujuzi wa kutosha lakini kwa upande wa Viwanda wenyewe wakiamini Wahitimu hao hawana mafunzo ya kutosha na uzoefu jambo ambalo limesababisha Wahitimu hao kushindwa kupata ajira katika maeneo mbalimbali.
Aidha Prof.
Karimuribo amesema kikao hicho ndio mwanzo wa kujadili mapungufu yaliyopo kati
ya Viwanda, Makampuni na Taasisi za Elimu ya Juu na namna ya kuboresha
mashirikiano ambayo yataweza kuwapa nafasi Wanafunzi wanapokuwa wanaendelea na
masomo kuweza kupata nafasi ya kujifunza kwa vitendo ili kuongeza ujuzi wao
utakao weza kuwasaidia kukabiliana na changamoto hiyo.
Prof. Karimuribo amesema Taasisi za Elimu ya Juu zina sehemu kubwa ya kuhakikisha zinawaruhusu watu kutoka katika Viwanda na Makampuni kushiriki kutoa mafunzo pale wanapokuwa wameandaa mafunzo yao kwani mbali na kufanya tafiti na kutoa machapisho Vyuo vya Elimu ya Juu huko mbeleni vinategemea Wahitimu wake kuweza kumiliki makampuni na Viwanda jambo litakalo wezesha kupata majibu sahihi na suluhisho katika tafiti zinazofanywa na Wanataaluma kutoka Vyuoni .
0 Comments