SUAMEDIA

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aondoa zuio la mikutano ya kisiasa

 Na Gerald Lwomile

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameondoa rasmi zuio la mikutano ya hadhara ya kisiasa nchini na kuwa sasa mikutano hiyo itafanyika kama Katiba ya nchi inavyosema.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza Ikulu Jijini Dar es Salaam (Picha TBC)

Rais ameondoa zuio hilo leo Januari 03, 2023 Ikulu Jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wake na viongozi wa vyama vya siasa na kusisitiza kuwa ni muhimu kuwepo kwa amani nchini.

Amesema ni wajibu wa Serikali kulinda mikutano hiyo ya kisiasa lakini pia ni wajibu wa vyama vya siasa kufuata taratibu zilizowekwa na kuwa ni muhimu kufanya siasa za kujenga na si kubomoa.

“Kwa sheria zetu ni haki kwa vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara……, kwa hiyo uwepo wangu mbele yenu hii leo nikuja kutoa ruhusa, kuja kutangaza kuwa lile tangazo la kuzuia mikutano ya hadhara sasa tumeliondoa” amesema Rais Dkt. Samia.

Aidha Rais ameonya matumizi ya lugha katika majukwaa ya kisiasa na kusema lugha za matuzi na kashfa si sahihi kisheria na hata mila na desturi za mtanzania na atakayekwenda kinyume na hayo basi sheria itachukua mkondo wake.

Akizungumzia suala la Katiba, Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema  kuwa yeye na chama chake kimedhamiria kukwamua mchakato wa marekebisho ya Katiba na kuwa bado kumeendelea kuwepo kwa majadiliano ili kujua nini kifanyike kuhusu jambo hilo.

Amesema Katiba itakayoundwa ni ya watanzania wote na si wanasiasa pekee na kuwa kutaundwa kamati ambayo itahusisha  makundi mbalimbali, na kuwa sasa madai ya muda mrefu ya wanasiasa yanaanza kushughulikiwa ili kuhakikisha kunakuwa na amani nchini.

Rais amefanya uamuzi huo kufuatia kupokea mapendekezo ya kikosi kazi maalumu kilichoundwa pamoja na mazungumzo yake na chama kimoja ambacho kilikataa kushiriki lakini ushiriki wao sasa unaleta matumaini mapya na maridhiano ya kitaifa, mkutano huo wa Rais umeshirikisha vyama vyote vya siaasa 19 na viongozi wakuu wa Serikali.

Post a Comment

0 Comments