Na Amina Hezron, Morogoro
Katika kukabiliana na Mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha
kukosekana kwa maji ya kutosha kwa ajili ya matumizi ya majumbani na
kuzalishia umeme nchini, imeshauriwa kuwepo kwa utaratibu wa uvunaji
wa maji ya mvua katika kipindi cha mvua za masika yatakayosaidia
pindi yatakapohitajika.
Ushauri huo umetolewa na Mratibu wa Utafiti na Machapisho kutoka
katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA, Prof. Japhet Kashaigili
wakati akizungumza na SUAMEDIA kuhusiana na namna ya
kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa maji.
Amesema tafiti zinaonesha kuwa maji yanapokuwepo katika kipindi cha
mvua kuna uwezekano wa kuhifadhiwa chini ya ardhi na kutumika pale
ambapo yatahitajika lakini wakati wa uhifadhi wake ni lazima
yahakikishwe yana ubora unaokubalika ili kuepusha kudhuru maji chini
ya ardhi kwa kuwa yakishadhurika hayawezi kutibiki kiurahisi.
“Uvunaji wa maji chini ya ardhi ni njia ya kipekee ya kukabilina na
majanga kama hayo ya upungufu wa maji lakini zoezi hili litafanywa vizuri
pale tu ambapo maji hayo yatafanyiwa tafiti, kufahamika yapo kiasi gani, yapo katika ubora gani na yanaweza kutumika kwa muda gani lakini pia
mipaka yake ikoje ili kuweza kuwekewa utaratibu mzuri wa matumizi
yake”, alisema Prof. Kashaigili.
Prof. Kashaigili amesema jambo hilo la uhifadhi wa maji chini ya
ardhi hufanyika nchini Afrika Kusini, Namibia lakini pia utafiti katika
bonde la maji ya chini ya ardhi la Makutupora mkoani Dodoma
umeonesha yawezekana kuvilia maji ya mvua kubwa chini ya ardhi kwa
kutumia utaalamu mbalimbali ambao unaweza kufanyika kwa kujenga
mabwawa madogo madogo ambayo yanaruhusu kuingiza maji taratibu
chini ya ardhi ama kwa kutumia visima.
Amesema utafiti uliofanyika unaonesha kuwa jambo hilo linawezekana
hivyo ni suala sasa la kuangalia namna ya kulitekeleza katika mikoa
mingine hata kwa kuchimba visima vya chini ya ardhi kikubwa ni
kujihakikishia kupitia tafiti.
“Wataalamu tuendelee kufanya tafiti zaidi ili kuweza kuishauri Serikali
namna bora ya kuweka maandalizi ya namna ya kukabiliana na matatizo
kama haya katika kipindi kingine”, alisema Prof. Kashaigili.
Aidha ameongeza kuwa ni wakati sasa wa kuwahamasisha na
kuwajengea uwezo wananchi juu ya uchimbaji wa visima ili waweze
kukabiliana na changamoto za upatikanaji wa maji na kutunza mazingira
ya mito.
“Tujitahidi kuwa na utaratibu mzuri wa kutunza vyanzo vya maji na
kupitia ofisi za Bonde Jumuiya ya watumia Maji na Serikali za Mitaa
kwenye maeneo yao kusimamia vyanzo vya maji ambapo kwa sasa
ukienda katika kipindi hiki cha kiangazi utakuta mifugo mingi inaingia
kwenye vyanzo hivyo na wanaathiri kwani mifugo inapokuwa mingi
sehemu moja inaathiri kingo za mto”, alisema Prof. Kashaigili.
0 Comments