NA:Winfrida Nicolaus
Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kwa kushirikiana na Taasisi ya Chuo Kikuu cha Nelson Mandela kilichopo jijini Arusha pamoja na wawakilishi kutoka Asasi mbalimbali za Kiserikali na zisizo za Kiserikali,Wakulima pamoja na Wajasiriamali wamekutana kujadili Sera ambazo zitahusiana na Kilimo Ikolojia, kilimo ambacho ni endelevu na kinachotunza Mazingira.
Hayo yamebainisha na Kaimu Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) kutoka Jijini Arusha Dkt. Efrem Njau ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye Warsha kwa ajili ya Mradi wa Kitovu cha Kilimo Ikolojia nchini Tanzania na Botanicals chini ya Ufadhili wa Macknight Foundation kutoka nchini Marekani iliyofanyika Kampasi Kuu ya Edward Moringe Sokoine SUA.
Amesema lengo la Warsha hiyo ni kuhusiana na Jukwaa la Sera linalolenga kutoa fursa kwa washikadau katika biashara ya Pembejeo za kibayolojia na kujadili juu ya masuala muhimu ya biashara ya pemebejeo za Kibayolojia ili kukuza matumizi yake kusaidia mabadiliko kuelekea Kilimo Ikolojia nchini Tanzania.
‘‘Kwa maana nyingine ambayo ni bora zaidi ni kwamba tunaenda kuangalia mfano suala zima la kutumia pembejeo zile ambazo ni za asili mfano Mboji, kutumia Viuatilifu vinavyotokana na vyanzo vya Asili zaidi kuliko vyanzo vya Viwanda hivyo basi tunataka kwenda kutengeneza bidhaa bora ili kwamba tukisafirisha mazao yetu yaweze kuwa na kiwango kidogo cha masalia’’, amesema Dkt. Njau.
Kwa upande wake Prof. Esron Karimuribo Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uzamili, Utafiti, Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalam amesema matokeo ya Kitafiti ni ya muhimu sana katika kuongoza Sera mbalimbali ambazo ni msaada mkubwa kwa Taifa hivyo wao kama Chuo cha SUA katika kuonesha wanathamini kazi za kitafiti wameamua kuwekeza katika Utafiti kwa kutumia mapato yao ya ndani na wameanza kazi hiyo miaka mitatu iliyopita mpaka sasa inaendelea.
Amesema wanaamini matokeo ambayo yanatoka kwenye Tafiti ndiyo yatakayotengeneza Sera nzuri na katika ufanyaji wa Tafiti zaidi ya kuchangia maarifa kuna zao lingine la muhimu ambalo ni Bunifu ambapo Sera hiyo au Mjadala huo unajikita katika kujadili namna gani matokeo ya tafiti pamoja na Bunifu yanaweza kubiasharisha.
Naye Prof. Anthony Sengada Mtafiti na Mkuu wa Mradi wa Kitovu cha Kilimo Ikolojia SUA amesema tafiti wanazozifanya katika Mradi anaouongoza ni tofauti na tafiti zingine ambapo kwa ushirikiana na wadau wa Kilimo Ikolojia nchini Tanzania ambao wanashugulika na wakulima waliojitoa na vilevile wapo mstari wa mbele katika kubadilisha Kilimo chao cha mazoea na kukifanya kuwa Kilimo cha Kiikolojia ama Kibailojia.
Ameongeza kuwa wamejikita katika Kilimo Ikolojia kwasababu Kilimo cha mazoea kimekuwa kikitumia Kemikali nyingi na kupelekea kuharibu Afya ya Udongo lakini pia Afya ya Walaji hivyo wanajaribu kufikiria kulima kilimo ambacho kina matumizi madogo ya mbolea za viwandani na iwe zaidi kwa kutumia Viuatilifu ambavyo ni vya Kibaiolojia.
0 Comments