NA GLADNESS MPHURU
Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) Prof. Charles Domminick Kihampa amekipongeza Chuo kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kutoa elimu kwa vitendo kama ambavyo muelekeo wa Serikali ya awamu ya sita inavyosisitiza.
Ameyazungumza hayo octoba 13, 2022 Kampasi kuu ya Edward Moringe mkoani Morogoro, kwenye ziara ya siku moja ya watumishi wa TCU, akiongozwa na mwenyeji wake Makamu Mkuu wa SUA Prof. Raphael Chibunda.
“Lengo la ziara hii ni kwaajili wafanyakazi wa Tume hii kuweza kuona Vyuo vilivyopo chini ya tume hiyo vinafanya nini, tunajua kuwa SUA ni Chuo kikubwa na kina maeneo mengi”
Prof. Kihampa ameyataja maeneo ambayo wameweza kuyatembelea katika ziara hiyo kuwa ni kitengo cha Samaki, Hospitali kuu ya Rufaa ya wanyama Tanzania ambapo wameweza kushuhudia operesheni ikiwa inaendelea pamoja na kituo atamizi ambapo ameweza kupongeza kuwa kituo hicho ni fursa kwaajili ya vijana wa kitanzania kuweza kujitegemea.
Aidha, ametoa rai kwa watanzania kuwa waendelee kuviamini vyuo vya ndani hususani SUA, kwasababu kimeendelea kufanya vizuri kwa kutoa wataalamu wenye ujuzi kwa miaka mingi.
“tumeoneshwa matrekta na mimi nikajua sasa wale wanaofundishwa Agriculture Engineering ni lazima ukitoka hapa chuoni unajua kuendesha trekta na kwa ile program jinsi ilivyo na matrekta 17 ambayo tumeyaona kwakweli nafikiri niseme tu kwamba vijana wanaosoma hapa wanabahati kubwa kuja kusoma sehemu ambapo wanapata ujuzi moja kwa moja zaidi ya nadharia” Alisema Kihampa
“nimshukuru tena makamu mkuu wa SUA Prof. Chibunda kwa kukubali ombi letu la kuja kuwatembelea tunajua kwamba alikuwa na majukumu mengi lakini ametuonesha yeye mwenyewe ametupitisha sehemu mbalimbali kwahiyo sisi tumefarijika sana na wafanyakazi wa TCU sasa wamejionea wenyewe” Alisema Kihampa
Awali Makamu Mkuu wa SUA Prof. Chibunda akiwakaribisha ameweza kuwapatia historia ya SUA kwa ufupi, amezitambulisha kampasi za SUA pamoja na shughuli zote zinazofanywa na SUA.
“Chuo chetu kina Kampasi 6 ambazo ni Kampasi Kuu ya Edward Moringe, Solomoni Mahlangu, Kampasi ya Olmotonyi Arusha, Kampasi ya Mazumbai Lushoto,Tanga katika msitu huu tuna miti yenye miaka zaidi ya 200 hadi 250, Kampasi ya Tunduru, Kampasi ya Mizengo Pinda Katavi na Shamba la Mti Ifinga yenye jumla ya hekari 10,000” Alisema Chibunda
0 Comments