SUAMEDIA

Ushirika wa Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUGECO umeombwa kuingia katika Sekta ya Mifugo

Na: Gojo Mohamed

Ushirika wa Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUGECO umeombwa kuingia katika Sekta ya Mifugo ili kuweza kuwapatia vijana ujuzi wa kutosha katika masuala ya ufugaji.

Mkurugenzi wa Uendeshaji na Ubunifu Bw.Joseph Massimba akimkabidhi Katibu Mkuu
Wizara ya Mifugo na Uvuvi Matunda aina ya Sweet Melon ambayo SUGECO wanazalisha katika
mashamba yao ya majaribio mkoani Morogoro

Ombi hilo limetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw.Tixon Nzunda wakati akitembelea Ushirika huo uliopo mkoani Morogoro na kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na SUGECO katika kuwainua vijana na wanawake hususani katika Sekta ya  Kilimo.

“Niwapongeze kwa kazi mnazozifanya kwa kuonesha uratibu mzuri na ushirikishwaji wa vijana katika Sekta ya Kilimo, naamini kwa namna nilivyoona nimeridhishwa na huduma zinazotolewa hapa lakini pia niwapongeze kwa kuendelea kuwalea vijana kujitambua, kujifunza na kuwa na elimu ya kujitegemea, sasa niwaombe na ninyi kuingia katika sekta ya mifugo na sisi tunawakaribisha mtusaidie kujenga uwezo katika vituo vyetu vya uatamizi”, amesema Bw. Nzunda.

Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuiunga mkono na kuweza kufanya kazi kwa ukaribu maana wanataka kutengeneza vituo vya uatamizi katika maeneo yote ya kupumzishia mifugo ili vijana waweze kujikwamua kiuchumi na itakuwa ni furaha  kuona SUGECO ikiingia katika sekta ya mifugo.

Kwa upande wake Bw. Joseph Masimba ambaye ni Mkurugenzi wa Uendeshaji na Ubunifu kutoka katika Ushirika huo wa SUGECO amesema kuwa ushirika huo unafanya shughuli mbalimbali ikiwemo kubadilisha mtazamo kwa vijana, mafunzo kwa vitendo, huduma za uatamizi pamoja na tafiti za ujasiriamali. 

“Nikushukuru Katibu kwa kuja kututembelea na kujionea pamoja na kujifunza shughuli mbalimbali tunazozifanya hapa SUGECO na tukuahidi kuwa tutaendelea kushirikiana na ofisi yako pamoja wataalamu wako kama nilivyosema tunaelekea kwenye ufugaji tutakuja na wazo pamoja na mradi ili tujadiliane na wataalamu wako ili tupate njia nzuri na kabla ya huu mwaka  kuisha tutakuja na wazo ambalo ni nzuri sana”, amesema Masimba. 








Post a Comment

0 Comments