Na: Winfrida Nicolaus
Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Peter Pinda ametoa rai kwa Serikali kuhakikisha wanazipa kipaumbele Tafiti zinazofanywa na Vyuo vikuu Tanzania ikiwemo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kila Mwaka ili kuisaidia jamii na kuleta Maendeleo kwa Taifa.
| Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Peter Pinda akiungumza na wananch wiakati wa Uzinduzi wa Maonesho ya 29 ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi Kanda ya Mashariki yanayofanyika Mkoani Morogoro. |
Mhe. Pinda amebainisha hayo Agosti 4, 2022 wakati wa Uzinduzi wa Maonesho ya 29 ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi Kanda ya Mashariki yanayofanyika Mkoani Morogoro.
Amesema Serikali inapaswa kuwapa kazi Vyuo Vikuu nchini ikiwezekana kila mwaka vikusanye Tafiti angalau tatu au tano ambazo wataziona zina tija kubwa katika kuleta mabadiliko kwa watanzania kwa kuwa Tafiti zinazofanywa zinatakiwa zionekane zinaenda mahali gani na zimesaidia jamii kwa kiasi gani.
Amesema kwenye Maonesho ya 29 ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi yenye lengo la kuelimisha jamii hasa katika Kilimo inaonesha ni kwa namna gani tafiti zinazofanywa na Vyuo kama SUA na vingine zina mambo makubwa na mazuri ambayo Serikali ikiyatumia na kuyapeleka kwa jamii itasaidia kuleta tija kwa Taifa.
“Tuna Vyuo kama SUA hawa watu ukienda na kusikiliza Tafiti zao wana mambo makubwa na mazuri na watakwambia katika tafiti liko hili na kwenye tafiti hii kuna hili lakini nadhani hata wao watakuwa wanajiuliza uliza sasa hizi tafiti zinasaidia wapi na kwa kiasi gani sasa nilikuwa nawaza kwanini hivi Vyuo tusiwape kazi mfano unawaambia SUA kila mwaka tuleteeni tafiti tatu au tano ambazo ninyi mnaona zina impact kubwa katika kuleta mabadiliko kwa Watanzania”, amesema Mhe. Mizengo Pinda
Aidha amevitaka Vyuo Vikuu vyote kupitia Tafiti zao kwenda Serikalini na kuelezea vitu ambavyo wamevifanyia Tafiti vilevile vina msaada gani kwa jamii ikiwa vitatumiwa ikiwemo Kilimo, Mifugo, Uvuvi na kuangalia ni namna gani vitaingizwa kwenye Mipango ya Serikali na kufanyiwa kazi.
Ameongeza kuwa Sekta ya Kilimo ni Muhimili Muhimu katika kuleta Maendeleo kwa Taifa hivyo ni vizuri kupima jamii imesaidika vipi kupitia Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi lengo likiwa ni kuhamasisha jamii na kuleta maendeleo kwa Taifa kupitia Kilimo, Ufugaji, Uvuvi pamoja na Misitu.
0 Comments