SUAMEDIA

Tumieni Tafiti na Teknolojia mpya kuongeza tija kwenye Kilimo- Mhe.George Simbachawene

 

Na Farida Mkongwe Kurunge

Wakulima, Wafugaji na  Wavuvi nchini wametakiwa kuzitumia Teknolojia mpya, Tafiti na Takwimu sahihi zilizotolewa wakati wa Maonesho ya Nanenane nchini kuongeza Tija katika Uzalishaji, Usindikaji, na Ubora wa Mazao ili kuifanya Sekta ya Kilimo kuchochea ajira, kukuza uchumi na kuongeza pato la wananchi na Taifa kwa ujumla.












Kauli hiyo imetolewa Agosti 8 mwaka huu na  Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Utawala Mh. George Simbachawene wakati akifunga rasmi Maonesho ya Nane nane Kanda ya Mashariki yaliyofanyika Mkoani Morogoro.


Mhe. Simbachawene amesema Kanda ya Mashariki inayo fursa nyingi zikiwemo za Viwanda na Uwekezaji hivyo kuwataka Wakulima, Wafugaji na Wavuvi kuzitambua fursa hizo lakini kwa Waoneshaji wa Maonesho hayo kuhakikisha wanafikisha kwa jamii Teknolojia zote zilizopo kwenye Maonesho yao.


“Rai yangu kwa Waoneshaji ni kutambua umuhimu wa Bunifu zenu na Teknolojia mpya kuhakikisha zinakuwa na manufaa kwa jamii, wote tulioshiriki tufanye tathmini ikiwemo uhalisia wa Teknolojia tunazozionesha kama ni kweli zipo na zinatumika kwenye maeneo yetu", amesema Mh. Simbachawene.

Awali akizungumza kabla ya Mgeni Rasmi Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Antony Mavunde amesema Wizara ya Kilimo nchini imejipanga kuikuza Sekta ya Kilimo kwa kwa asilimia 10 kufikia mwaka 2030 kwa kuongeza Uzalishaji katika Kilimo cha Umwagiliaji na kuviwezeha vituo vya Utafiti kufanya utafiti wa Mbegu bora.


Mikakati mingine ni pamoja na kuziwesha Maabara kupima udongo ambapo kwa kuanzia tayari wameshapima udongo kwa mikoa 18 ya Tanzania ili kuwafanya Wakulima waachane na kilimo cha kubahatisha.

“Mwaka huu Serikali imeongeza bajeti ya Kilimo kutoka sh. Bilioni 294 mwaka 2021/2022 na kufikia bilioni 954 kwa mwaka 2022/2023 ili kufikia azma hiyo ya kukikuza Kilimo kwa asilimia 10 kufikia mwaka 2030", amesema Naibu Waziri.

Katika hotuba yake Mh. Mavunde pia ametoa Rai kwa Viongozi wa mikoa ya Kanda ya Mashariki kuhakikisha wanatenga maeneo ya kilimo kwa ajili ya vijana na kwamba Serikali ipo tayari kushirikiana nao katika kuhalikisha Sekta ya Kilimo inachangia kupunguza tatizo la ajira nchini na kujenga Maghala kwa ajili ya kuzuia upotevu wa mazao baada ya kuvunwa.


Katika Maonesho hayo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kimeibuka Mshindi wa kwanza katika kundi la Vyuo Vikuu na Vyuo vya Kati huku ikiibuka Mshindi wa pili wa jumla ambapo mshindi wa kwanza ni Bodi ya Sukari Tanzania.

 

KATIKA PICHA : SUA kimeibuka Mshindi wa kwanza katika kundi la Vyuo Vikuu na Vyuo vya Kati huku ikiibuka Mshindi wa pili wa jumla ambapo mshindi wa kwanza ni Bodi ya Sukari Tanzania.






 

Post a Comment

0 Comments