SUAMEDIA

Afya Data ubunifu wa SUA mfumo unaosaidia kupunguza madhara yatokanayo na magonjwa ya Mlipuko

 

NA:Farida Mkongwe

Imeelezwa kuwa Mfumo wa Afya Data ambao umebuniwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kuwa ni mfumo ambao unasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza madhara yatokanayo na magonjwa ya Mlipuko.



Hayo yameelezwa na Dr. Robert Andrew Maduka ambaye ni Mratibu Msaidizi wa Mradi unaojishughulisha na Tafiti za Magonjwa Ambukizi ya Binadamu na Wanyama SACIDS wakati akizungumza na SUAMEDIA kwenye viwanja vya Maonesho ya 29 ya Nanenane Kanda ya Mashariki yanayofanyika Mkoani Morogoro.

Dr. Maduka amesema mfumo huo wa Afya Data unatumika kutoa taarifa za dalili za magonjwa ya mlipuko ambapo watu waliopo kwenye maeneo yenye dalili za magonjwa hayo wanawasiliana na watoa huduma za afya kwa kutuma ujumbe wa dalili wanazoziona na baadae watoa huduma za afya wanafuatilia na kubaini tatizo

“Mfumo huu unaweza ukaupakua na ukawa nao kwenye Simu yako ya mkononi, ukishakuwa nao basi ni rahisi kuripoti taarifa za dalili za magonjwa ya milipuko iwe kwa binadamu au wanyama kwa maana ya mifugo”, amesema Dr. Maduka.

Akizungumzia faida za mfumo huo Mratibu huyo amesema licha ya  kusaidia kufikisha taarifa za magonjwaya mlipuko kwa haraka lakini pia unasaidia watu wengi kushiriki kutoa taarifa kwa sababu kabla ya mfumo huo kuna watu walikuwa hawajui pahali sahihi pa kufikisha taarifa licha ya kujua matatizo yaliyopo kwenye jamii zao.

Amesema kwa sasa mfumo huo bado upo kwenye uangalizi na kazi katika wilaya mbalimbali zikiwemo Kilosa, Malinyi, Mvomero, Gairo, Ulanga na Ngorongoro ambapo tayari mafunzo yameshatolewa kwa watoa huduma za afya ngazi ya jamii ya namna ya kutumia mfumo huo na kuzifanyia kazi taarifa zinazotolewa.

Post a Comment

0 Comments