NA: Farida Mkongwe
Maabara inayotembea
iliyopo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kwa kiasi kikubwa imechangia
kudhibiti magonjwa ya mlipuko kutokana na Maabara hiyo kuwa na uwezo wa
kuyafikia maeneo yenye ugonjwa kwa haraka.
Hayo yamebainishwa na
Dkt. Edson Kinimi ambaye ni Mhadhiri, Idara ya Fiziolojia, Biochemia na Famakolojia
iliyopo Ndaki ya Tiba ya Wanyama na Sayansi za Afya SUA wakati akizungumza na
SUAMEDIA katika viwanja vya Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki
yanayofanyika mkoani Morogoro.
Dkt. Kinimi amesema
tangu kuanza kutumika kwa Maabara hiyo kumekuwa na unafuu kwa Serikali na
Wananchi kwa ujumla kwa sababu kumekuwa na uwezo wa kuyadhibiti kwa haraka
magonjwa ya milipuko.
“Hili gari lina uwezo wa
kwenda sehemu korofi ambazo hazifikiki kiurahisi hata nyakati za mvua, gari
hili lina uwezo wa kufika sehemu hizo na kwa sababu lina vifaa vinavyosaidia
kujua vinasaba vyenye magonjwa yanayosababishwa na Virusi, Bakteria au magonjwa
ya Kuvu basi vipimo vinafanywa na majibu kupatikana hapo hapo”, amesema
Mhadhiri huyo.
Akizungumzia chimbuko la
Ubunifu wa Maabara hiyo inayotembea, Dkt. Kinimi amesema dhana hiyo imekuja
baada ya kuwepo kwa magonjwa ya milipuko na kuwepo ugumu wa kuyafikia maeneo
husika.
“Ubunifu wa hii Maabara
inayotembea umetokana na kutaka kufika maeneo husika ambayo yanakuwa na
maambukizi hivyo tukafikiria namna ya kufika maeneo husika ili tuweze kufanya
uchunguzi na kutoa majibu kwa haraka’, amefafanua Dkt. Kinimi.
Ameongeza kuwa wakati wa
ugonjwa wa Korona waliweza kufanya kazi na Wizara ya Afya na Taasisi ya Taifa
ya Utafiti na kusaidia kwa mara ya kwanza kubaini vinasaba vya ugonjwa wa
Korona.
“Na juzi juzi tu
ulisikia habari ya homa ya Mgunda chuo cha SUA kimeweza kuhusika kupima kupitia
Taasisi yake ya SACIDS”, amesema Dkt.Kinimi.


0 Comments