SUAMEDIA

Wanafunzi SUA watengeneza njia kwa ajili ya watalii katika Bustani ya Miti na Maua SUA, Morning Site Morogoro Manispaa

 

Na: Gojo Mohamed

Wanafunzi wa Shahada ya Kwanza katika Kozi ya Utalii Mapumziko Uishi kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wametengeneza njia ya watembea kwa miguu kwa ajili ya watalii pamoja na kutambua maeneo tofauti ya kupumzikia maarufu kama Camp Site katika bustani ya miti na maua yanayomilikiwa na SUA katika eneo la Morning Site Manispaa ya Morogoro.


PICHA NA MTANDAO

Mhadhiri kutoka Idara ya Utalii na Mapumziko Uishi SUA aliyekuwa akisimamia na kuratibu shughuli hizo Bw. Semi Thadeo Mokiti amesema kuwa mambo makubwa ambayo wanahusika nayo ni kuwaandaa vijana kuweza kuja kuwa wabunifu, wasimamizi na waongozaji wa masuala ya utalii

Amesema wanafunzi hao wa mwaka wa kwanza na baadhi yao   kutoka mwaka wa pili na wa tatu wamechukua hatua ya kuyatambua na kutengeneza maeneo ya kupumzikia karibu na lango kuu la kuingia SUA ili kufufua maeneo hayo kwa ajili ya shughuli za kiutalii chuoni hapo.

‘‘Kwa Mwaka huu wa 2022 katika mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wetu tumekuwa na programu maalumu na hii ni moja ya harakati ya kumuunga mkono Rais wetu Mhe. Samia Suluhu Hassan kuendeleza utalii katika nchi yetu na tulianza na kutengeneza njia kwa ajili ya watalii kupita katika bustani ya ‘Bortanical Garden’  iliopo karibu na lango kuu  la kuingia  SUA na kazi nyingine ni kuliendeleza eneo la Morning Site ’’. Amesema Mokiti

Ameongeza kuwa licha ya wanafunzi kutengeneza njia kwa ajili ya watalii wanaofika SUA pia wamefanikiwa kuanzisha camp site tatu mpya ambazo ni rasmi na za kuvutia kwa ajili ya watu kupumzika

Kwa upande wake Mwanafunzi Gudluck Tukai amesema kuwa amejifunza vitu vingi akiwa darasani na hata nje ya darasa ambapo amejifunza na kufanya kwa vitendo hivyo amewashauri wanafunzi wenzake katika kozi hiyo kufanya mazingira yawe yanavyotakiwa

Naye Neema Lazaro amesema kupitia kazi walioifanya ya kufufua maeneo kwa ajili ya utalii amejifunza namna ya kuandaa mazingira ambayo yatawafanya watalii waweze kuvutiwa zaidi kutembelea maeneo ya utalii ikiwemo SUA Chuo ambacho kinatoa mafunzo kwa nadharia pamoja na vitendo


 

Post a Comment

0 Comments