Na Editha Mloli
Ukuaji wa Sekta ya Kilimo kila siku unatokana na watu kuendelea kupata elimu ya namna ya kulima kitaalam na kupata mazao mengi na yenye tija ambapo kutokana na hilo, jamii nchini imeshauriwa kujikita katika uzalishaji wa migomba kwa njia ya chupa kwani ina faida lukuki kwa mkulima.
![]() |
| PICHA MTANDAO |
Ushauri huo umetolewa na Mtaalam wa Magonjwa ya Mimea Dkt. Hellen Kanyaga kutoka Idara ya Mimea Vipando na Mazao ya Bustani iliyopo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA wakati akizungumza na SUAMEDIA.
Dkt. Hellen amesema kwa miaka ya hivi karibuni watu wamekuwa na mwitikio mkubwa wa kuzalisha migomba kwa njia ya chupa kutokana na faida mbalimbali ikiwa ni pamoja na uzalishaji wa miche mingi kwa wakati mmoja tofauti na uzalishaji wa kawaida au wa kienyeji uliozoeleka.
Ameongeza kuwa miche hii ya migomba inayozalishwa kwa njia ya chupa kutoka Maabara inakuwa hainyemelewi na magonjwa kutokana na uangalizi mkubwa unaofanywa na wataalam kuanzia uzalishaji hadi mavuno.
“Tunafanya hivi kwa sababu ina faida sana ikiwemo kupata migomba safi isiyokuwa na magonjwa ambapo kwa hatua inayopitia hadi kukua kama itakuwa na magonjwa basi itagundulika mapema lakini siyo hivyo tu, pia tunazalisha migomba mingi kwa wakati mmoja ambapo unaweza kuzalisha kwa ajili ya hekta moja na ukapanda yote kwa wakati mmoja na ikakua yote pamoja”, amesema Dkt. Hellen
Akielezea kuhusiana na namna ya kuzalisha migomba hii kwa njia ya chupa amesema kuwa wanachukua chipukizi la mgomba wowote ambao mkulima atahitaji wenye afya na kuuchonga kati ya mizizi na ile sehemu ya katikati ya mgomba ili kupata tishu inayohitajika ambayo kitaalam inaitwa Melistem tissue.
Dkt. Hellen ameongeza kuwa kama Mkulima ataamua kuzalisha migomba kwa njia ya chupa anatakiwa kufuata kanuni bora za uzalishaji na utunzaji na akitumia mbegu iliyo bora ana nafasi nzuri ya kufanikiwa katika zao hili la migomba.
“Huwa tunasema ukianza na mbegu bora ni lazima huko mbele mazao yanakuwa mazuri kama ukianza na mgomba msafi na una uhakika hauna viini vyovyote vya magonjwa maana yake kwamba kama utautunza vizuri na kufuata kanuni bora za kilimo mwisho wa siku unategemea mazao mazuri na kwa vile ni msafi unakuwa na tabia ya kukua haraka”
Ameongeza kuwa migomba inayozalishwa kwa njia ya chupa ina tabia ya kukua kwa haraka tofauti na ile inayozalishwa kwa njia ya kawaida kwa kuwa hii inayozalishwa kitaalam ina uhakika wa kukua kuanzia miezi tisa hadi mwaka mmoja na miezi miwili kwa kutegemea na aina ya mgomba.
Aidha Dkt. Hellen amewataka wataalam kuzalisha kwa wingi miche hii ya migomba kwa njia ya chupa kwani wakulima wanaohitaji huduma hii wamekuwa wakiongezeka kila siku.

0 Comments