Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro amewataka Watumishi wa Umma nchini kutumia namba ya simu 26 2160240 ya Kituo cha Huduma kwa Mteja ya Ofisi ya Rais-UTUMISHI kuepuka gharama za kusafiri hadi jijini Dodoma kwa lengo kufuatilia na kutatua changamoto za masuala ya kiutumishi zinazowakabili.
Dkt. Ndumbaro ametoa wito huo leo, mara baada ya kushiriki utoaji wa huduma kwa watumishi wa umma na wananchi kupitia Kituo cha Huduma kwa Mteja (Call Center) cha Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Dkt. Ndumbaro amesema, kwa watumishi wanaokabiliana na changamoto za kiutumishi katika maeneo yao ya kazi badala ya kuingia gharama za kusafiri kuja jijini Dodoma kutatua changamoto zao za kiutumishi, ni vema wakapiga simu hiyo ya Kituo cha Huduma kwa Mteja ili wapewe huduma kwani watumishi wa kituo hicho wapo tayari kuwahudumia.
“Tumieni namba ya simu ya kituo cha Huduma kwa Mteja cha Ofisi ya Rais-UTUMISHI ili kupunguza gharama na kurahisisha ushughulikiaji wa changamoto za kiutumishi zinazowakabili,” Dkt. Ndumbaro amesisitiza.
Ameongeza kuwa, mtumishi wa umma anaweza kusafiri umbali mrefu kuja jijini Dodoma halafu akakuta anayemfuata amuhudumie hayupo katika kituo cha kazi hivyo akaingia gharama ya nauli na kujikimu wakati angetumia namba ya simu angehudumiwa bila gharama yoyote.
Dkt. Ndumbaro amesema kuwa, kituo hicho cha huduma kwa mteja kinaondoa viashiria na uwepo wa vitendo vya rushwa kwani huduma kwa watumishi inatolewa kwa njia simu, hivyo kuepuka malalamiko ya vitendo vya rushwa ambavyo kwa asilimia kubwa vinababishwa na matapeli wenye nia ya kujiingizia kipato kupitia changamoto zinazowakabili watumishi wa umma.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro ametoa huduma kupitia Kituo cha Huduma kwa Mteja (Call Center) cha Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, 2022.
0 Comments