SUAMEDIA

SUA kupitia Kurugenzi ya Huduma za Hospital imetoa mafunzo kuhusu Afya ya Uzazi kwa wanafunzi

 Na Amina Hezron

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kupitia Kurugenzi ya Huduma za Hospital kimetoa mafunzo kuhusu afya ya uzazi kwa wanafunzi ili kuepukana na mimba zisizotarajiwa, maambukizi ya virusi vya ukimwi na magonjwa mengine yanayoenezwa kwa njia ya ngono isiyo salama.

Akizungumza katika mafunzo hayo Mlezi wa Wanafunzi SUA ambaye alikuwa Mgeni rasmi kwenye mafunzo hayo Pule Mutashabi amesema kuwa Familia na Serikali zimewekeza katika suala la elimu ili kuhakikisha vijana wanapata ujuzi wa kuweza kusaidia familia zao.

Amesema pamoja na uwekezaji huo ipo hatari kwa ndoto hizo kufutika kutokana na athari za mimba zisizotarajiwa na magonjwa ya zinaa ukiwemo Ukimwi.

“Matumaini yangu kuwa ninyi mliopata fursa hii ya kujifunza kwa undani masuala ya kuhusu afya ya uzazi mtafikisha ujumbe sahihi kwa wenzenu kwa weledi mkubwa hivyo nawaomba mtumie fursa hii kuuliza maswali mbalimbali kwa lengo la kujifunza kikamilifu”, amesema Mutashabi.

Aidha amewataka wanafunzi hao kuwa mabalozi wazuri katika mapambano dhidi ya UKIMWI, magonjwa ya ngono na kupunguza uwepo wa mimba zisizotarajiwa na kuhakikisha kuwa wahitimu wa SUA wanahitimu kwa wakati wakiwa na afya njema tayari kwa kulitumikia taifa na pia kutimiza ndoto zao.

Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkazi wa hospitali za SUA Elimwidimi Swai amesema kuwa wao kama wataalamu wa afya wameona umuhimu wa kuwakumbusha wanafunzi kuhusiana na afya ya uzazi na changamoto zilizopo kwakuwa wanafunzi wa Vyuo Vikuu katika umri walio nao wapo hatarini katika kupata changamoto zitokanazo na afya ya uzazi. 

“Lengo rasmi ni kutoa elimu ili waweze kuelewa namna bora ya kushughulika na afya ya uzazi ikiwemo Uzazi wa Mpango pamoja na kuelewa magonjwa ambayo yanaweza kuambukizwa kwa njia ya ngono na namna ya kujikinga”, alisema Swai.

Kwa upande wake Muuguzi Mkuu kutoka hospitali ya SUA  Deograsia Sigura amewataka wanafunzi waliopata nafasi ya kupokea mafunzo hayo kwenda kuyaishi yale waliojifunza na  kuwa walimu wazuri kwa wenzao ili wakaweze kujikinga na magonjwa ya zinaa.

Mmoja wa wanafunzi waliopata mafunzo hayo Jacob Christopher ameipongeza hospitali ya SUA kwa kuandaa mafunzo hayo yatakayowasaidia vijana kujua namna bora ya kujikinga na magonjwa pamoja na mimba zisizotarajiwa


    










Post a Comment

0 Comments