SUAMEDIA

Watendaji kutaneni na wananchi moja kwa moja na si kukalia vikao na posho tu - Msando

 

Na Gerald Lwomile

Serikali wilayani Morogoro imepiga marufuku vikao vya kupeana posho na kupiga porojo tu na  inataka kuona vikao kazi na ushiriki wa moja kwa moja kwenye maeneo husika ambavyo vitaleta manufaa kwa wananchi na taifa kwa ujumla.


Mkuu wa wilaya ya Morogoro, Albert Msando akizungumza wadau wa kilimo na uhifadhi wa mazingira

Zuio hilo limetolewa Juni 2, 2022 na Mkuu wa wilaya ya Morogoro, Bw. Albert Msando wakati akifungua Kikao Kazi cha Maandalizi ya Jukwaa la Mazingira na Kilimo Endelevu na Shirikishi, kikao kilichaanza Juni 2 katika Manispaa ya Morogoro na kinatarajiwa kukamilika Juni 4, 2022.

Msando amesema kumekuwa na tabia kwa watendaji wengi kushiriki  katika vikao vyenye posho na porojo tu na kushindwa kwenda kwenye maeneo husika kutatua changamoto mbalimbali katika sekta ya kilimo, ufugaji, uvuvi na uhifadhi wa mazingira.

Akizungumzia uharibifu wa mazingira katika maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na wilaya ya Morogoro, Msando amesema hivi sasa wananchi wengi wana elimu na uelewa kuhusu mazingira na kinachosababisha uharibifu ni pamoja na mahitaji muhimu ya kibinadamu.


Wadau wa kilimo na uhifadhi wa mazingira wakimsikiliza Mkuu wa wilaya ya Morogoro Albert Msando hayuko pichani

Ametolea mfano mahitaji ya viwanja kwa ajili ya ujenzi wa makazi na gharama kubwa ya upatikanaji wa viwanja hivyo kuwa ni moja ya sababu za watu kujenge milimani na pembezoni mwa mito wakati sheria inatawa makazi yajengwe kuanzia mita 60 na kuendelea pembeni mwa mto na hivyo sasa inahitajika njia mbadala za kukabiliana na changamoto hizi.

“…., sasa kama huyu mtu hataweza kumudu gharama za ununuzi wa kiwanja atatafuta sehemu rahisi ili amudu gharama na maeneo haya rahisi ni viwanja vilivyoko kwenye milima yetu ambapo kuna vyanzo vya maji” Amesema Msando.

Msando amesema njia hizi mbadala ni pamoja na Manispaa na Halmashauri kuhakikisha zinatenga maeneo ambayo kila mwananchi atamudu kupata eneo linaloweza kumsaidia kutimiza mahitaji muhimu ya kibinadamu ikiwa ni pamoja na  kuwa na makazi.

Akizungumzia Kikao Kazi cha Maandalizi ya Jukwaa la Mazingira na Kilimo Endelevu na Shirikishi, Meneja wa Kongani ya Kilombero (SAGCOT) Bw. John Banga Nakei amesema mpango  wa Kongani hilo tangia limeanza umekuwa ukiangalia uhusiano uliopa kati ya wakulima wadogo, wakubwa na wadau wengine na uhifadhi wa mazingira kwa namna ya kipekee


Meneja wa Kongani ya Kilombero (SAGCOT) John Banga Nakei akizungumza na washiriki wa kikao kazi

Banga amesema Mabadiliko ya Tabia Nchi  imekuwa sehemu ya mpango wa SAGCOT katika kuhakikisha kunakuwa na kilimo, ufugaji na uvuvi endelevu huku wadau katika sekta hizo wakikabiliana na changamoto hii ya mabadiliko ya tabia nchi

Post a Comment

0 Comments