Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania – TFS Prof. Dos Santos Silayo ametoa wito kwa wataalamu wa sekta ya misitu Barani Afrika kufanya tafiti na kuzichapisha kwenye machapisho yanayokubalika duniani ili kufikisha ujumbe wa tafiti hizo kwa jamii.
Prof. Silayo amesema hayo Jumatatu Juni 20, 2022 mara baada ya kufungua warsha ya wataalamu wa sekta ya misitu wakiwemo watafiti na waadhiri wanaotoka katika nchi 15 Barani Afrika zinazoongea lugha ya kiingereza.
Kamishna wa Uhifadhi - TFS, Prof. Silayo alikuwa mgeni rasmi kwenye warsha hiyo iliyoandaliwa na Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) kwa kushirikiana na Jukwaa la Wadau wa Misitu Afrika (AFF) na Chuo cha Kilimo Sokoine (SUA).
Prof. Silayo anasema taarifa zinaonyesha kuwa maeneo mengi Barani Afrika tafiti nyingi zinafanyika kweye taasisi za kitafiti na tasisi za elimu ya juu lakini haziwekwi katika utaratibu wakuwafikia watumiaji.
“Tafiti nyingi zinafanyika lakini haziwafikii watumiaji, huku ni kupoteza rasilimali muda na fedha zinazotumika aidha kuwafundisha wataalamu ama fedha zinazotumika kwa ajili ya kukusanya taarifa ambazo zilipaswa kuchakatwa na kuwekwa katika mfumo ambao utakaoweza kuwafikia watumiaji kirahisi ili ziweze kuleta matokeo chanya katika sekta ya misitu na sekta inayohusiana na masuala ya uhifadhi wa misitu,” anasema Prof. Silayo.
Charles Meshack, Mkurugenzi wa Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) anasema wameamua kufanya warsha hiyo ya siku tano baada ya kubaini uwepo wa changamoto kubwa kwa wanasayansi wachanga wa sekta ya misitu katika kuchapisha tafiti zao kwenye majarida ya kimataifa.
Anasema kupitia warsha hiyo washiriki watapatiwa mafunzo yatakayolenga kuwajengea uwezo wa kuhakikisha wanachapisha tafiti zao si kwa ajaili ya wanayayansi tu bali hata kwa watoa maamuzi.
“Lengo kubwa la warsha hii ni kuhakikisha kwamba wanasayansi washiriki wanapewa mafunzo yakuweza kuhakikisha wanachapisha, na mafunzo haya yanaangalia jinsi wanavyofanya utafiti, utaratibu wanatumia kufanya utafiti, jinsi ya kuangalia matokeo na jinsi ya kuyaangalia matokeo kwa ajili ya kuyawasilisha kwa watoa maamuzi,
“Mara nyingi watu wamekuwa wakiandika kwa ajili ya masuala ya taaluma pekee na changamoto kubwa wanashindwa kuonyesha nini msoma hiyo ripoti anapaswa kufanya. Hivyo kupitia warsha hii wataenda kufundihwa namna ya kuandika ili msomaji wa mwisho aweze kufanya maamuzi,” anasema Meshack.
Kwa upande wake Prof. Godwin Kawero Katibu Mkuu wa Jukwaa la Wadau wa Misitu Afrika (AFF) anasema katika mafunzo hayo wataanza kuwakumbusha namna bora ya uandishi wa kisayansi na kisha uandishi kwa ajili ya makundi yote utakaozingatia uandishi wa lugha nyepesi inayoeeleweka.
Jumla ya wanasayasi 25 watapatiwa mafunzo hayo huku mafunzo mengine yakitarajiwa kufanyika kwa nchi za Afrika zinazozungumza lugha ya kifaransa siku za karibuni.
0 Comments