SUAMEDIA

Uwepo wa Waandishi wa Habari wa kiraia ambao hawana sifa za uandishi wageuka kikwazo kwa waandishi.

 

Na.Vedasto George.

Imeelezwa kuwa uwepo wa Waandishi wa Habari wa kiraia ambao wanatumia mitandao ya kijamii kusambaza taarifa kwenye jamii bila ya kuwa na sifa za uandishi wa habari umechangia kuwepo kwa upotoshaji wa taarifa jambo linalopelekea Tasnia ya Habari kuzidi kudharaulika  licha ya kuwa  ni sekta muhimu nchini.

 


Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa  Habari Mkoa wa Morogoro Nicksoni Mkilaya kwenye  Kongamano la  Maadhimisho ya  Uhuru wa Habari Duniani ambapo amesema waandishi wa habari za kiraia ambao si wanataluma wamekuwa wakisababisha upotoshaji mkubwa wa taarifa kwa kuwa wengi wao hawana uweledi wa taaluma hii ya uandishi wa habari

 

Nicksoni Mkilaya Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa  Habari Mkoa wa Morogoro akitoa hotuba yake katika Kongamano la  Maadhimisho ya  Uhuru wa Habari Duniani iliyofanyika katika ukumbi wa  New Savoy hotel mjini Morogoro.

Aidha amewataka Waandishi wa Habari kuendelea kuibua kero  zinazoikabili jamii zikiwemo za kiafya na kiuchumi pia amewaomba wana Habari kote nchini kutokubali kuwa wanyonge kwa kuwa ni watu mahili  kutoka katika taaluma mahili  na nyeti.

 

Kwa upande wake mgeni rasmi Mh. Abdulaziz Abood ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Morogoro amesema mabadiliko ya Teknolojia  ya Habari na mawasiliano yasitumike kama kichaka cha  kufanya uhalifu na kusababisha kuwepo kwa mmomonyoko wa maadili kwenye jamii badala yake teknolojia itumike katika kutangaza shughuli za kiuchumi ili kuleta chachu ya maendeleo katika jamii.

 

Pia amesema mabadiliko ya kidigitali yasiangaliwe kwa mtazamo hasi bali yaangaliwe kama fursa ya teknolojia ili itumike kusaidia wanafunzi wanaosoma kwenye Sekta ya Habari  na Mawasiliano ya umma nchini pindi watakapo hitimu masomo yao.

 

Kongamano la Maadhimisho ya Uhuru wa Habari Duniani hufanyika kila mwaka ifikapo Mei 3 ambapo kwa mkoa wa Morogoro Maadhimisho hayo yamefanyika tarehe 9, Mei 2022, yakiwa na kauli mbiu isemayo “Uandishi wa Habari na Changamoto za Kidigitali”.

 




Post a Comment

0 Comments