SUAMEDIA

Nape Akemea Matajiri Kutumia Fedha Majina Ya Mitaa

 


 


WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari amesema si sahihi kwa matajiri kutumia fursa ya kuwajengea watu miundombinu au kutoa fedha kidogo ili mitaa iitwe majina yao.


Nape alisema anafahamu kuna baadhi ya maeneo yana migogoro ya majina na kubainisha kuwa hakuna mtaa utakaochaguliwa jina na serikali, hivyo vifanyike vikao vya serikali za mitaa na wakazi wote wa eneo husika wakubaliane jina la mtaa husika.


Alisema hayo jana Dodoma alipohojiwa katika kipindi cha Jambo Tanzania kinachorushwa na chaneli ya TBC1 ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).


“Nataka pia niweke wazi kuwa majina ya mitaa yanayotokana na makubaliano ya wakazi wenyewe, lakini nimesikia kuna baadhi ya mitaa kuna watu wanaweka miundombinu au wanatoa fedha ili mitaa iitwe majina yao, nadhani hii sio sawasaswa,” alisema Nape.


Alisema jambo hilo likiachiwa liendelee akipatikana tajiri anaweza akaweka mtaa mzima majina yake na kutaka iangaliwe namna ambayo itahakikisha majina ya mitaa yanaakisi asili ya eneo husika au watu wake.


“Tunayo majina mengi ya viongozi na mashujaa wetu, kabila na miji yetu haya ndio yawe majina ya kipaumbele badala ya kuita mitaa mtu mwenye fedha. Tunaweza kukuta mji mzima tajiri mmoja ameweka majina ya watoto wake,” alibainisha.


Aidha, alitaka taasisi za serikali ikiwemo Wakala ya Barabara Tanzania (Tanroads) na Wakala ya Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura), kutumia nafasi ya uwekaji wa anuani za makazi na postikodi kuweka majina katika barabara zake zote inazojenga ili kuurahisishia mfumo huo.


“Tutumie nafasi hii tuweke majina ya barabara zetu, na taasisi nyingine kama vile Shirika la Taifa la Nyumba (NHC) na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kila mmoja ashiriki na kuweka anuani kwenye eneo lake. Kila Mtanzania aone ni ufahari kuwa na anuani ya makazi,” alisisitiza Nape.


Akizungumzia utaratibu mzima wa uwekaji anuani za makazi na postikodi, alisema unaendelea vizuri na hadi jana ulikuwa umefikia asilimia 67 nchi nzima huku lengo likiwa ukamilike Mei, mwaka huu.


“Tunatakiwa hadi Mei 22, mwaka huu, mfumo uwe umekamilika, kama tunakwenda kwa sasa kwa zaidi ya asilimia 50 maana yake tuko zaidi ya asilimia 67 kazi inakwenda vizuri maana yake tunaweza tukaukamilisha mwezi huu, mwezi ujao ukawa ni kusafisha tu taarifa na mwishoni mwa mwezi tukamkabidhi Rais Samia Suluhu Hassan ripoti,” alieleza Nape.


Aidha, alieleza kwamba kulikuwa na changamoto katika mfumo ambayo wataalamu wanashughulikia iliyotokana na mashine ya kupokea taarifa kuzidiwa kutokana na wingi wa taarifa zilizokuwa zinakwenda kwa wakati mmoja.


Alisema tatizo lingine lilikuwa la kitaalamu kwa maana ya watu mikoani walikopewa kazi baadhi yao walikuwa wanapata changamoto ya kutumia teknolojia ya kisasa, lakini sasa wamepelekwa wataalamu wengi mikoani ili kutatua changamoto ya ujuzi.


Alieleza kuwa kazi inakwenda vizuri ingawa iko mikoa inafanya vizuri zaidi na iko mikoa bado inasuasua kwa sababu ya kutoanza kwa zoezi kwa wakati.


“Na mwezi huu, ikiwezekana tutaongeza nguvu zaidi ikiwezekana tukamilishe kazi mwezi huu na mwezi ujao uwe ni wa kusafisha taarifa tulizozipokea ili itakapofika Mei mwishoni tumkabidhi Rais mfumo ukiwa umekamilika,” alisema Nape.


Kuhusu kutoa elimu, alisema serikali imejitahidi kutoa elimu kuhusu utaratibu huo wa uwekaji anuani za makazi na postikodi, lakini alikiri kuna baadhi ya maeneo kuna changamoto ya watu kuuliza maswali ya msingi yaliyopaswa kuwa yameshajibiwa tangu mwanzo.


Alitoa wito kwa vyombo vya habari nchini kusaidia kutoa elimu kuhusu uwekaji huo wa anuani za makazi kwani ni ya nchi nzima na inamhusisha kila Mtanzania na itabadilisha namna ambavyo maisha yao yanaendeshwa.


“Kila Mtanzania popote alipo kwenye eneo la kazi, makazi unakofanyia biashara kama halijawekewa namba au anuani yako ya mtaa nenda kwenye serikali yako ya mtaa toa taarifa,” alisema Nape.


Alielezea faida za utaratibu huo kuwa ni kubwa ikiwemo huduma kurahisishwa kupatikana, usafirishaji wa vifaa na mizigo mbalimbali kurahisishwa na kumtafuta mtu au eneo itakuwa ni rahisi kupatikana.

Post a Comment

0 Comments