SUAMEDIA

Watafiti nchini wametakiwa kufuata taratibu zote za kisayansi kwa ili kuzalisha matokeo bora

Na Farida Mkongwe

Watafiti nchini wametakiwa kuhakikisha wanafuata taratibu zote za kisayansi ili matokeo ya tafiti hizo yaweze kuwa bora ikiwa ni pamoja na kushirikiana na Wizara na Sekta mbalimbali zinazotumika katika utungaji wa sera.

Rasi wa Ndaki ya Sayansi za Jamii na Insia Prof. Samweli Kabote kutoka SUA wakati akifungua Warsha ya wadau ya kujadili namna bora ya matumizi ya tafiti kwenye utungaji wa sera za nchi.

Wito huo umetolewa Machi 17, 2022 mjini Morogoro na Rasi wa Ndaki ya Sayansi za Jamii na Insia Prof. Samweli Kabote wakati akifungua Warsha ya wadau ya kujadili namna bora ya matumizi ya tafiti kwenye utungaji wa sera za nchi.

Prof. Kabote amesema kwa muda mrefu hapa nchini kumekuwa na changamoto ya namna ya kuzitumia tafiti katika kuleta maendeleo na kwamba ili tafiti hizo ziweze kutumika ipasavyo ni lazima kuwepo na muunganiko kati ya matokeo ya tafiti pamoja na watunga sera.

“Tunachosisitiza hapa kwenye workshop hii ni kuboresha matokeo ya tafiti zetu na kuwa na mfumo mzuri wa kuweza kuwasiliana na watunga sera ili waweze kutumia matokeo ya utafiti katika kuandaa sera ambazo zinajibu changamoto za watu vijijini na mijini”, amesema Prof. Kabote.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti Mafunzo na Huduma za Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Angello Mwilawa amesema kupitia warsha hiyo watatoa mchango na kushauri jinsi tafiti hizo zitakavyofika kwa wavuvi na wafugaji ili waweze kuongeza uzalishaji na ubora katika shughuli zao.

“Hapa tulipo ni Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA ni Chuo chetu Kikubwa Tanzania kinachojishughulisha na tafiti, na tafiti nyingi zimeshafanyika sasa ni kuangalia tu namna zitakavyowafikia wananchi”, amesema Dkt. Mwilawa

Naye Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Upanzi Misitu kutoka Lushoto ambacho kipo chini ya Taasisi ya Utafiti wa  Misitu Tanzania Dkt. John Mbwambo amesema ili matokeo ya tafiti yaweze kuwafikia na kueleweka kwa jamii ni vizuri ikatumika lugha rahisi inayoeleweka na wengi.

“Kwa mfano tafiti nyingi sana zimefanyika lakini watafiti au wanasayansi wamekuwa wakiwajulisha wanasayansi au watafiti wenzao, lugha inayotumika ni ya kisayansi hivyo jamii au mtumiaji wa chini hawezi kuelewa umuhimu wa tafiti hizo”, amesema Dkt. Mbwambo.

Warsha hiyo imehitimisha mafunzo ya siku mbili ya Watafiti kutoka SUA na Watafiti kutoka nchini Denmark ambayo yalilenga kujengeana uwezo wa namna ya kutumia matokeo ya kisayansi katika kushawishi jamii pamoja na watunga sera katika kufanya mabadiliko yatakayoleta maendeleo ya wananchi.

 


Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti Mafunzo na Huduma za Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Angello Mwilawa akizungumza mara baada ya Warsha ya wadau ya kujadili namna bora ya matumizi ya tafiti kwenye utungaji wa sera za nchi.

Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Upanzi Misitu kutoka Lushoto ambacho kipo chini ya Taasisi ya Utafiti wa  Misitu Tanzania Dkt. John Mbwambo  akielezea umuhimu wa Taasisi yake kushiriki katika Warsha ya wadau ya kujadili namna bora ya matumizi ya tafiti kwenye utungaji wa sera za nchi.
Picha ya  pamoja watafiti kutoka SUA na Denmark, wadau kutoka Wizara ya Kilimo Wizara ya Mifugo na Uvuvi na watafiti wa Taasisi za kitaifa za kitafiti


Post a Comment

0 Comments