SUAMEDIA

Wataalamu wa Mawasiliano amkeni mtafute taarifa zitakazotatua changamoto walizonazo wananchi

 

Calvin Gwabara

Dar es Salaam

Wataalamu wa masuala ya Menejimenti ya Maarifa na Maafisa Mawasiliano nchini  wametakiwa kuamka kutafuta maarifa hayo kutoka kwenye maeneo mbalimbali yanakozalishwa na kuyafikisha kwa jamii ili yakajibu changamoto zinazoikabili jamii katika kukuza uchumi wao na Taifa.

 Meneja wa Mawasiliano na Menejimenti ya Maarifa kutoka Taasisi ya Utafiti Tanzania (TARI) Dkt. Richard Kasuga wakati akiwasilisha mada yake

Wito huo umetolewa na Meneja wa Mawasiliano na Menejimenti ya Maarifa kutoka Taasisi ya Utafiti Tanzania (TARI) Dkt. Richard Kasuga wakati akiwasilisha mada yake kuhusu Menejimenti ya Maarifa nchini hasa katika sekta ya kilimo kwa maafisa menejimenti ya maarifa na mawasiliano kutoka katika taasisi mbalimbali za utafiti, vyuo vikuu na maeneo mengine.

“Maarifa yapo mengi sana kwenye vituo vyetu vya utafiti,vyuo vikuu na maeneo mengine yanayozalisha maarifa lakini jamii yetu hasa wakulima hawawezi kufika kuzifuata na kuzitafuta huko lakini sisi kama wataalamu wa menejimenti ya maarifa tunaweza kwenda kuzichimbua na kuwaletea wananchi wetu kuzitumia na kubadilisha maisha yao. Alisema Dkt. Kasuga.

Dkt. Kasuga amesema kwenye kurasa za taasisi mbalimbali ikiwemo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kupitia Mkulima Library, Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania TARI, TARIRI, Mamlaka ya Hali ya Hewa, NIMRI na nyingine nyingi kumewekwa maarifa mbalimbali wanayozalisha ambayo yanahitajika na wakulima na wafugaji hivyo ni jukumu la wataalamu hao wa mawasiliano na menejimenti ya maarifa kuzitembelea na kuchukua yanayohitajika ili jamii ikayatumie.

Pichani ni washiriki wa mkutano huo ambao ni maafisa menejimenti ya maarifa,mawasiliano kutoka taasisi mbalimbali nchini.

Meneja huyo wa menejimenti ya maarifa na mawasiliano wa TARI ameongeza kuwa siku hizi zipo njia nyingi za kufikisha maarifa kwa jamii ambazo jamii inazitumie ikiwemo mitandao ya kijamii,kama vile twitter, facebook, Instagram lakini pia Televisheni, Redio na Magazeti ambazo wanaweza kuzitumia kufikisha  elimu kwa walengwa kirahisi.

Tanzania inaendesha mafunzo  ya kitaifa ya siku nne ya kuwajengea uwezo Maafisa Mawasiliano, Wagani na Waandishi wa Habari namna ya kuchakata matokeo ya Tafiti na kuwafikishia walengwa sambamba na kufuatilia na kutoa taarifa za utekelezaji wa maazimio ya Malabo ulioandaliwa na Taasisi ya Uratibu wa Tafiti za Kilimo (CCARDESA) kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI).

 


 

 

Post a Comment

0 Comments