SUAMEDIA

Wanafunzi wa darasa la tano kutoka Shule ya Msingi Safepa watembelea SUA

 Na Editha Mloli

Wanafunzi wa darasa la tano kutoka katika Shule ya Msingi Safepa wametembelea Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kwa lengo la kujifunza mambo mbalimbali yanayofanyika Chuoni hapo hususani katika Idara ya Mawasiliano na Masoko, Kitengo cha SUAMEDIA kinachorusha matangazo ya moja kwa moja ya redio.


Wanafunzi kutoka Shule ya Msingi Safepa wakipata maelekezo jinsi ya kurusha na kupata taarifa mtandaoni kutoka kwa Mwanahabari Farida Mkongwe walipotembelea SUA kwa lengo la kujifunza mambo mbalimbali yanayofanyika.



Akizungumza mara baada ya ziara hiyo Mwalimu wa shule hiyo aliyeambatana na Watoto hao Kalenzi Pius amesema wanafunzi hao wamechagua Chuo Kikuu cha SUA kwa ajili ya kujifunza namna ambavyo vipindi vya redio vinaendeshwa Chuoni hapo.

Amesema mapendekezo ya Watoto kufanya ziara SUA ni ili kuwapa motisha ya kufanya bidii zaidi katika masomo yao na kuweza kufikia hatua ya kusoma Chuo Kikuu cha SUA kwani ndiyo matamanio ya Watoto wengi katika kufikia malengo yao.


Aidha mwalimu Kalenzi ametoa shukrani kwa uongozi pamoja na wafanyakazi wa SUAMEDIA kwa mapokezi mazuri waliyoyapata kwani imewapa nafasi ya kufahamu mambo mengi yanayofanyika ndani ya SUA FM.


“Tumekuja hapa SUA Fm leo na Watoto wa darasa la tano kwa ajili ya Watoto kujifunza namna redio na vipindi vinavyoendeshwa na ni kwa sababu ni mapendekezo kutoka kwa Watoto kuja SUA kwa kuwa kuna Chuo na Redio kwa kuwa wazazi pia tuna ndoto za Watoto wetu siku moja kufika Chuo Kikuu na zaidi wawe na bidii kwenye masomo ili waweze kufika Chuo Kikuu”,  amesema Mwalimu Kalenzi.


Kwa upande wao wanafunzi waliopata nafasi ya kufika Chuoni hapa wamesema lengo lililowafanya kuja SUA FM ni pamoja na kufahamu matangazo ya redio yanarukaje kutoka chumba cha kurushia matangazo hadi kuwafikia majumbani kupitia radio zao.


Wanafunzi hao wametoa wito kwa Watoto wengine kufika katika  Chuo Kikuu cha SUA ili kujifunza mambo mengi ambayo yanafanywa na Chuo ikiwa ni pamoja na Redio,  Masomo yanayofundishwa chuoni hapo na Miradi mbalimbali inayotekelezwa SUA.


Wanafunzi kutoka Shule ya Msingi Safepa wakisikiliza maelezo ya namna ya kurusha matangazo ya Redio kutoka kwa Mtangazaji wa Kipindi cha Kapu la leo Hadija Zahoro walipotembelea SUA FM RADIO.
Katika picha ya pamoja Wanafunzi kutoka Shule ya Msingi Safepa, Walimu wa shule Safepa na watangazaji wa SUFM Radio.

Post a Comment

0 Comments