Na: Farida Mkongwe
Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA na Watafiti kutoka nchini Denmark wamekutana katika warsha ya mafunzo ya siku mbili kwa lengo la kujengeana uwezo wa namna ya kutumia matokeo ya kisayansi katika kushawishi jamii pamoja na watunga sera katika kufanya mabadiliko yatakayoleta maendeleo ya wananchi.
Akifungua Warsha hiyo mjini Morogoro Machi 16, 2022 Mkurugenzi, Kurugenzi ya Uzamili,
Utafiti, Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalam kutoka SUA Prof. Esron
Karimuribo amesema mara nyingi watafiti wamekuwa wakifanya tafiti nyingi lakini
kumekuwa na changamoto ya namna ya kuwasilisha tafiti hizo kwa wananchi na
watunga sera.
“Ni tukio ambalo kwetu tunaliona ni muhimu sana, mara nyingi
watafiti wetu wamekuwa wakifanya tafiti tu katika maeneo tofauti ambayo yamelenga
kuboresha maisha ya wananchi, lakini jinsi gani ambayo wanawasilisha kwa
walengwa inakuwa ni changamoto, kwa hiyo warsha hii inalenga kujenga uwezo wa
watafiti katika kutoa ushauri mzuri kulingana na matokeo ya utafiti”, amesema
Prof. Karimuribo
Prof. Karimuribo amesema baada ya warsha hiyo ya siku 2
kumalizika watakutana na wadau wengine kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara
ya Kilimo, pamoja na Taasisi za Kitaifa za Kitafiti ili kujadili jinsi ya
kutumia uwezo wa watafiti kisayansi katika kuboresha maisha ya wananchi
wakiwemo wakulima na wafugaji.
Kwa upande wake Mratibu wa Mradi wa Kujenga Uwezo kwa Vyuo
Vikuu BSU Prof. Antony Sangeda amesema Mradi
huo ambao umegawanyika katika awamu tatu umekuwepo Chuoni hapo kwa muda wa miaka
10 mfululizo ambapo awamu ya kwanza wamefanikiwa kuongeza elimu kwa watafiti wa
SUA na kufanya mafunzo ya aina mbalimbali.
“Katika awamu ya pili tumetengeneza Mitaala kwa ngazi ya Masters na PhD ambapo tumepata mitaala mitatu ambayo imeshaidhinishwa na
kupata ithibati ya Tume ya Vyuo Vikuu Nchini,TCU, na inatekelezwa na ina
wanafunzi lakini kwa awamu hii ya tatu ambayo tunaelekea mwisho wa Mradi huu tunaamini
uwezo wa SUA ambao umejengwa utakuwa endelevu ili kusaidia tafiti zetu kutoa
majawabu kwa changamoto za wananchi”, amesema Prof. Sangeda.
Mradi huo wa Kujenga Uwezo kwa Vyuo Vikuu ambao umefadhiliwa na
Shirika la
Maendeleo la Kimataifa la Denmark (DANIDA) utafikia tamati mwezi Desemba mwaka
huu.
Mratibu wa Mradi wa Kujenga Uwezo kwa Vyuo Vikuu BSU Prof. Antony Sangeda |
0 Comments