SUAMEDIA

Serikali yapokea maombi ya kujiunga na Taasisi ya Africa50

 



Na. Ramadhani Kissimba na Eva Valerian, WFM - Dodoma

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ameiahidi Taasisi ya Africa50 kuwa Serikali imepokea maombi ya kuitaka Tanzania kujiunga na Taasisi hiyo na mapendekezo hayo yatafanyiwa kazi ndani ya Wizara na Serikali na baadae kuyafikisha maombi hayo kwenye Mamlaka ya juu kwa ajili ya kufanya maamuzi.


Mhe. Dkt. Nchemba aliyasema hayo jijini Dodoma alipokutana na ujumbe wa Taasisi ya Africa50 ukiongozwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi hiyo Bw. Alain Ebobisse’, ambapo aliwapongeza kwa miradi wanayotekeleza ambayo kwa Tanzania ni miradi ya kipaumbele.

“Tumefurahishwa na miradi mnayotekeleza ya sekta za uzalishaji zikiwemo kilimo, nishati, mifugo na uvuvi ambayo na kwetu sisi, Serikali na nchi kwa ujumla ni miradi ya kipaumbele ambayo inayosimamiwa kikamilifu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Samia Suluhu Hassan. “. Alisema Mhe. Nchemba.

Mhe. Nchemba aliongeza kuwa dira ya Serikali ni kuweka nguvu kubwa kwenye sekta za uzalishaji ambazo zinachochea ukuaji wa sekta nyingine mfano uzalishaji wa nishati ya umeme na gesi, ambapo uzalishaji wa bidhaa hiyo unapaswa kupewa kipaumbele na kufanyiwa uchambuzi ili kuangalia uwezekano wa kushirikiana na  Taasisi  ya Africa50 katika kuendeleza sekta hiyo kupitia njia ya ubia  kati ya Serikali na Sekta binafsi.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi hiyo Bw. Alain Ebobisse’ alisema kuwa dhamira yao kubwa ni kushirikiana na Tanzania na kuwa ipo tayari kuisaidia  kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo hasa ile inayotekelezwa kupitia ubia kati ya serikali na sekta binafsi.

Pia Bw. Ebobisse’ alitumia fursa hiyo kuiomba Tanzania kujiunga na Taasisi hiyo ambayo ilianzishwa kwa lengo la kusaidia, kufadhili na kuhamasisha sekta ya Umma na binafsi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Mhe. Mwigulu alimuhakishishia Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Africa50 kuwa Serikali itakaa na kuchambua baadhi ya miradi ambayo inaweza kukidhi vigezo ili Serikali iweze kushirikiana na Taasisi hiyo kwa njia ya ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi ili kuweza kuwafungulia fursa vijana wa Tanzania ambao ndio wengi kushiriki katika utekelezaji wa miradi hiyo jambo litakasaidia kukuza ajira kwa vijana na  kuongeza kipato kwa nchi na kwa mtu mmoja mmoja.

Post a Comment

0 Comments