Na: Mohamed Gojo
Wanafunzi wanaosoma Vyuo Vikuu wametakiwa kuzingatia mafunzo
wanayofundishwa kwa vitendo kwa kuwa mafunzo hayo ndio yatakayo wanufaisha mara
baada ya kumaliza masomo yao.
Wito huo umetolewa na Mhadhiri wa Idara ya Lishe ya Binadamu na Sayansi ya Mlaji katika Ndaki ya Kilimo iliyopo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Mary Marcel wakati akizungumza na SUAMEDIA kuhusu umuhimu wa mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi.
Akizungumza kuhusu maonesho ya ubunifu yaliyofanywa na
wanafunzi wa mwaka wa pili na wa tatu wanaosoma Shahada ya Sayansi ya Familia
na Mlaji amesema mafunzo hayo kwa vitendo yatawasaidia wanafunzi hao kujiajiri
hasa kwa wakati huu ambapo Tanzania inazungumzia uchumi wa viwanda
“Tunaelewa Tanzania sasa inaelekea kuwa Tanzania ya Viwanda na Rais wetu ameshaonesha kuwa tunataka kufufua viwanda kwa hiyo ujuzi watakaoupata sasa utawasaidia kuishi hali ya Taifa ya kuelekea kwenye viwanda….”, alisema Mhadhiri huyo.
Kwa upande wao baadhi ya Wanafunzi wanaosoma Shahada hiyo ya
Sayansi ya Familia na Mlaji Juliana Maina na Fred James wamesema mafunzo hayo
yanawasaidia kuwa wabunifu na kupata ujuzi ambao watautumia baada ya kuhitimu
masomo yao.
Katika Maonesho hayo wanafunzi wameonesha ujuzi na ubunifu wao
kwa kutengeneza viti kwa kutumia matairi ya magari, bajaji na pikipiki, maua
kwa kutumia matawi ya miti yaliyodondoka pamoja na mapambo mbalimbali.
0 Comments