Na Hadija Zahoro
Wakulima nchini wametakiwa kuvijua na kuvitofautisha Viwavijeshi kulingana na misimu ili waweza kupambana navyo katika misimu yote ya kilimo.
Wito huo umetolewa na Mtafiti Mwandamizi wa Viuatilifu na Visumbufu Maneno Chidege kutoka Taasisi ya Kutafiti na Kudhibiti Visumbufu vya Magonjwa ya mimea, magugu na wadudu pamoja na Kemikali zinazotumika kwenye mazao ya kilimo TPRI iliyopo jijini Arusha.
Akizungumza mubashara katika kipindi cha Mseto Moto kinachorushwa na SUAFM, Chidege amesema walipata sampuli za wadudu wa Viwavijeshi vamizi mwezi Machi, 2017 wenye muundo wa funza ambao wanatoboa mahindi baada ya kuingia katikati ya shina la muhindi ambapo wakulima wakadhani ni ugonjwa wa sulenge au mbenya.
Amesema kuna tofauti kubwa kati ya Viwavijeshi vinavyoibuka kati ya mwezi Februari na Machi kila mwaka, ambavyo wakulima wamevizoea vyenye madoa meusi na vile Viwavijeshi vamizi vinavyoibuka mwaka mzima katika misimu yote ya kilimo.
Kutokana na hali hiyo Mtafiti huyo amewataka wakulima kutumia viuatilifu vya mfumo kuua aina ya Viwavijeshi vamizi ambavyo vina tabia ya kujificha katika mahandaki ya mimea.
‘‘Viuatilifu vya mfumo akiwa amejificha ndani ukipulizia inaenda kumuua kwa sababu inaenda kuingia kwenye mwili wa mmea kwa sababu mmea unapumua kama sisi binadamu tunavyopumua, lakini akiwa juu ya mmea unapaswa kutumia kiuatilifu cha mguso ambapo ukipulizia tu ule mvuke ukimpata anakufa’’, alisema Maneno Chidege
Kutokana na wakulima kukosa uelewa kuhusu uvamizi wa viwavijeshi shambani, Chidege amesema TPRI wamebuni mfumo ambao unaonesha picha na viashiria mbalimbali vya kuvamiwa na wadudu hao ili wajue aina gani ya kiuwatilifu kinachoweza kuwatokomeza kabisa.
0 Comments