SOURCE MUUNGWANA BLOGMuda mfupi baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kukutana na
kufanya mazungumzo na Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), Tundu Lissu viongozi mbalimbali wamepongeza hatua hiyo.
Rais Samia na Lissu walikutana jana Jumatano Februari 16, 2022
mjini Brussels nchini Ubelgiji na kuteta masuala mbalimbali yenye maslahi ya
ustawi wa Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano
ya Rais-Ikulu, Zuhura Yunus wawili hao walikutana baada ya ombi la Lissu la
kukutana na Rais, ombi ambalo mkuu huyo wa nchi aliliridhia.
Muda mfupi baada ya Ikulu kutoa taarifa za viongozi hao
kukutana, Lissu ambaye alikuwa mgombea urais katika Uchaguzi Mkuu 2020 kupitia
Chadema alitaja mambo matano aliyosema wameyazungumzia na Rais Samia likiwamo
kesi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chedema, Freeman Mbowe na wenzake
watatu.
Hata hivyo, baada ya taarifa za Rais Samia na Lissu kukutana
kusambaa kupitia mitandao ya kijami ikiwamo ya Mwananchi, watu mbalimbali
walielezea mapokeo yao kuhusu viongozi hao kukutana.
Baadhi ya waliozungumzia suala hilo ni pamoja na viongozi wa
Serikali wakiwamo mawaziri.
Kupitia akaunti zao za mitandao ya kijamii wakiweka picha
zikimuonyesha Rais Samia akiwa amesimama pamoja Lissu huku wakiambatania na
maneno 'captions' wamesema;
"NI MAMA YETU (Taifa letu, Umoja Wetu)" ameandika
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba katika ukurasa wake wa Twitter
akiwa ameambatanisha picha tatu za Rais Samia akiwa na Lissu.
Kwa upande wake Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kupitia mtandao
wa Instagram akiwa ameweka picha ya Rais Samia amesimama na Lissu wakiwa
wameshikana mkono, amesema “My President, My Pride. This is Tanzania (Rais
wangu, Fahari Yangu, Hii ni Tanzania)”
Andiko la Waziri Ummy liliungwa mkono na Naibu Spika wa Bunge
la Tanzania, Mussa Zungu ambaye aliweka maoni ‘comment’ kwenye posti hiyo
akisema “Excelling Diplomacy (Diplomasia bora)”
Mwingine aliyezungumzia hilo ni Mkuu wa Wilaya ya Morogoro
(DC), Wakili Albert Msando ambaye kupitia ukurasa wake wa Instagram amesema
“Tuna Rais bora sana. Hatumlinganishi na yeyote. Sio lazima. Kila mmoja ana
kipawa chake. Mh. Mama Samia Suluhu Hassan tutamuelewa tukitaka kuelewa.
#Legacy” ameandika Msando
Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema kuwa
hatua ya Rais Samia kukubali kukubali kukutana na Lissu ni ya kupongezwa
“Hatimaye hekima imetawala na mlango wa mazungumzo umefunguka. Sisi
@ACTwazalendo tokea awali tunasisitiza kwamba mazungumzo ndiyo njia sahihi ya
kupata ufumbuzi wa tofauti zetu za kisiasa na kuleta Mabadiliko. Hatua ya Rais
kukubali kuonana na Bwana Lissu ni ya kupongeza sana” ameandika Zitto
Mbunge wa zamani wa Arusha Mjini ambaye ni mwanachama wa
Chadema, Godbless Lema kupitia ukurasa wake wa Twitter amesema “Nimefurahi Rais
SSH kukutana na Makamu Mkti wetu Tundu Lissu. Kukutana kwao kuna jenga
matumaini ktk siku za usoni. Ninajua watakuwa wamejadili kwa kina hali ya nchi
yetu na changamoto zake kwa sasa na njia nzuri ya kuzivuka.”
Ameandika Mbunge huyo wa zamani wa Arusha Mjini kupitia
ukurasa wake wa Twitter.
0 Comments