Na Winfrida Nicolaus
Chuo Kikuu cha Sokoine Cha Kilimo SUA pamoja na Chuo Kikuu cha “Central University of Technology CUT (Free State) cha Afrika Kusini, kimefanya mkutano kwa ajili ya kuanzisha ushirikiano katika kuendesha mafunzo kwa kubadilishana wakufunzi pamoja na wanafunzi toka pande zote mbili baina ya Tanzania na Afrika Kusini kwa lengo la kuboresha mafunzo yanayoendeshwa na taasisi zote mbili.
Wajumbe
kutoka Afrika Kusini na Menejimenti ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA wakiwa
katika picha ya pamoja. |
Mkutano huo umefanyika Januari 31, 2022, katika Chuo Kikuu Cha Sokoine Cha Kilimo SUA Kampasi Kuu ya Edward Moringe Sokoine.
Bw. Bernard Matsoso Afisa Maendeleo katika Chuo Kikuu cha Kati cha Teknolojia cha Afrika Kusini amesema mkutano huo umelenga kuanzisha ushirikiano na Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki ili kuondokana na dhana ya ushirikiano hafifu baina ya Nchi za Afrika katika kukuza mitaala ya Elimu hususani katika ufanyaji wa tafiti.
Aidha amesema kutokana na ushirikiano huo wanafunzi pamoja na Wakufunzi kutoka pande zote mbili wanaweza kubadilishana uzoefu kwa kuwa wanakusudia kuanzisha Taasisi ya Kiswahili ambapo italeta faida kubwa kwa nchi ya Afrika Kusini katika kujifunza lugha ya Kiswahili kutoka kwa wazungumzaji wazawa.
‘‘Ili kukuza Mitaala ya elimu tunahitaji kufanya kazi karibu zaidi na Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki kama SUA, pia tumeangalia suala zima la kukiboresha Kiswahili katika nchi za Afrika ambapo nchi kama Tanzania na Kenya wamekuwa wakifanya vizuri katika lugha ya Kiswahili na sisi kama Afrika ya kusini bado tunajikongoja hivyo tunahitaji kujifunza Zaidi’’. Amesema Bernard Matsoso
Kwa upande wake Prof. Esron Karimuribo ambaye ni Mkurugenzi katika Kurugenzi ya Uzamili, Utafiti na Ushauri wa Kitaalam SUA amesema ushirikiano huo utalenga katika kufanya tafiti ambazo zina hisia na zina mlengo wa kuendeleza ushirikiano mzuri ambao utaleta changamoto chanya hasa kwa nchi za Afrika.
‘‘Nchi ya Afrika Kusini ni nchi ambayo kwa muda mrefu ilikuwa chini ya ubaguzi wa rangi lakini kwa sasa wanabadili mwelekeo wa kuwawezesha waafrika kuweza kushiriki katika elimu lakini katika maendeleo ya nchi zote mbili na tunaamini kwa namna hii kwamba tutaweza kushirikiana vema na kuweka mifumo mizuri ya makubaliano’’, amesema Prof. Karimuribo
Kikao hicho kimeazimia kuwa kuanzishwa kwa ushirikiano huo baina ya taasisi hizo mbili kutaleta mafanikio kwenye maeneo mengi ya kitaaluma na hivyo wameona ni wakati muafaka kushirikiana na kuweza kuboresha mitaala itakayokuwa na maudhui yaliyotengenezwa kwa kuakisi mazingira halisi ya kiafrika.
Wawakilishi
kutoka Chuo Kikuu cha “Central University of Technology Cut” (Free State) cha
Afrika ya Kusini wakifatilia kwa makini majadiliano wakati wa Kikao na
Menejimenti ya Chuo Kikuu cha SUA |
0 Comments