Na Gerald Lwomile
Katavi
Imeelezwa kuwa uzingatiaji wa maadili katika sehemu za kazi hujenga dhana za Uzalendo, Utaifa, Nidhamu, Uvumilivu na Utendaji na ufanisi wa kazi jambo linaloweza kuleta utoaji bora wa huduma na kuleta maendeleo katika taifa.
Hayo yamesemwa katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Kampasi ya Mizengo Pinda Mkoani Katavi na Mkuu wa Kanda ya Sekretarieti ya Maadili Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Bw. Paulo Kanoni wakati akizungumza na watumishi katika kampasi hiyo. Mafunzo hayo yameratibiwa na Kamati ya Kuthibiti Uadilifu (KKU) ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo.
Bw. Kanoni amesema endapo watumishi watazingatia maadili na kutoa huduma bora basi watajenga imani ya wananchi kwa serikali yao na Taasisi za umma.
“Uadilifu hujenga dhana za Uzalendo, Utaifa, Nidhamu, Uvumilivu na Utendaji na ufanisi wa kazi pia unasababisha matumizi mazuri ya Rasilimali za Umma” amesema Kanoni
Aidha amesema kuwa maadili mema katika maeneo ya kazi ni chimbuko la kufanikiwa kwa maendeleo ya sekta nyingine za kijamii kama elimu, maji, umeme, miundombinu na nyinginezo.
Naye Afisa Taasisi ya Kuzuia na Kupamabana na Rushwa (TAKUKURU) wilaya ya Mlele Mkoa wa Katavi Joseph Mwamkenda
amesema watumishi wengi wamekuwa wakikiuka maadili na kujikuta wakiingia katika
vitendo vya rushwa na hongo kutokana na kutaka kuishi maisha zaidi ya kipato chao.
Amesema kuwa rushwa ya ngono limekuwa
tatizo kubwa na hasa katika Taasisi za Elimu ya Juu na kupelekea sifa mbaya kwa
taasisi hizi katika jamii.
Amesema kifungu cha 28
cha sheria za TAKUKURU kinazuia ubadhilifu na ufujaji wa mali za umma na ni kosa
kutumia mali ya umma kwa matumizi binafsi.
Awali akifungua mafunzo hayo kwa watumishi wa Kampasi ya Mizengo Pinda, Rasi wa Ndaki wa Kampasi hiyo Prof. Josiah Katani alisema Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kina matumaini makubwa kuwa watendaji kazi katika Chuo hicho watafanya kazi kwa uadilifu na nidhamu ili kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wanafunzi, wananchi na taifa kwa ujumla.
Amesema SUA inatamani kuona wafanyakazi katika chuo hicho wanakuwa waadilifu na wenye nidhamu katika maeneo ya kazi na kutumia vizuri rasilimali za Chuo kwa kuzingatia kanuni na miongozo iliyowekwa.
Prof. Katani amesema SUA inatamani kuona watumishi wanakuwa na uhusiano mwema baina yao na wazingatie kuwa kila mtumishi anao mchango katika kuboresha utendaji kwenye eneo lake la kazi.
“Ni matarajio yangu mtakwenda kuwa waadilifu na wenye nidhamu katika maeneo yenu ya kazi lakini pia mtatumia vizuri rasilimali za Chuo kwa kuzingatia kanuni na miongozo iliyopo” Amesema Prof. Katani
Katika hatua
nyingine wafanyakazi katika Kampasi ya Mizengo Pinda wamekula kiapo cha
uadilifu kazini ambacho kimeongozwa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo
Usevya wilaya ya Mpimbwe Mh. Vulstan Kundy.
Rasi wa Ndaki ya Mizengo Pinda Prof. Josiah Katani anayeonekana mbele na wafanyakazi wa Ndaki hiyo wakila Kiapo cha Udilifu |
0 Comments