Kumekuwa na makabiliano makali kati ya wajumbe wa Urusi na Marekani katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, baada ya Marekani kuitisha mkutano wa kujadili kuhusu upelekwaji wa wanajeshi wa Urusi kwenye mipaka yake na Ukraine.
Balozi wa Marekani Linda Thomas-Greenfield alisema upelekwaji huo ulikuwa mkubwa zaidi Ulaya kuwahi kuonekana katika miongo kadhaa.
Mwenzake wa Urusi aliishutumu Marekani kwa kuchochea hali ya wasiwasi na uingiliaji usiokubalika katika masuala ya Urusi.
Marekani na Uingereza zimeahidi vikwazo zaidi iwapo Urusi itaivamia Ukraine.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza Liz Truss alisema sheria inatayarishwa ambayo italenga pande nyingi zaidi kuliko sasa dhidi ya watu binafsi na wafanyabiashara walio karibu na serikali.
Afisa mmoja wa Marekani alisema vikwazo vya Washington vinamaanisha kuwa watu walio karibu na serikali wataondolewa kwenye mfumo wa fedha wa kimataifa.
Urusi imeweka takriban wanajeshi 100,000, vifaru, mizinga na makombora karibu na mipaka ya Ukraine.
PICHA
Katika kikao cha Jumatatu cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Balozi wa Urusi Vasily Nebenzya alisema hakuna uthibitisho kwamba Urusi inapanga kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Ukraine, na kwamba kuongezeka kwa wanajeshi wake hakukuthibitishwa na Umoja wa Mataifa.
Alisema Urusi mara nyingi inahamisha wanajeshi katika ardhi yake na kwamba hilo haliihusu Marekani.
Urusi ilijaribu kuzuia kikao cha wazi cha baraza la Umoja wa Mataifa lakini ilishinda kwa kura 10 dhidi ya mbili.
Bi Thomas-Greenfield alisema Marekani inaendelea kuamini kuwa kuna suluhu la kidiplomasia lakini akaonya kwamba itachukua hatua madhubuti ikiwa Urusi itaivamia Ukraine, matokeo ambayo yatakuwa "ya kutisha".
"Huu ndio uhamishaji mkubwa zaidi wa wanajeshi barani Ulaya katika miongo kadhaa," alisema.
"Na tunapozungumza, Urusi inatuma vikosi na silaha zaidi kuungana nao."
Aliongeza kuwa Urusi ilikuwa inapanga kuongeza kikosi chake kilichotumwa katika nchi jirani ya Belarus, kwenye mpaka wa kaskazini mwa Ukraine hadi 30,000.
Jumatatu, Marekani iliamuru kuondoka kwa familia wa wafanyikazi wa serikali ya Marekani kutoka Belarus, kufuatia mkusanyiko usio wa kawaida na unaohusu jeshi la Urusi . Agizo kama hilo lilitolewa mwezi uliopita kwa familia za wafanyakazi wa serikali ya Marekani katika ubalozi wake mji mkuu wa Ukraine, Kyiv.
Wakati huo huo juhudi za kidiplomasia zinaendelea, huku Bw Putin akiongea kwa simu na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron siku ya Jumatatu.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken atafanya mazungumzo na waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov leo Jumanne.
Marekani inasema imepokea jibu la kuandikwa kutoka kwa Urusi kuhusu pendekezo la Marekani linalolenga kupunguza mzozo wa Ukraine.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje alisema kuwa Marekani imejitolea kikamilifu katika mazungumzo na itaendelea kushauriana kwa karibu na washirika wake ikiwa ni pamoja na Ukraine.
Urusi inataka nchi za Magharibi kuahidi kuwa Ukraine kamwe haitajiunga na muungano wa Nato - ambapo wanachama wanaahidi kusaidia wengine katika tukio la shambulio - lakini Marekani imekataa takwa hilo.
Wanachama 30 wa Nato ni pamoja na Marekani na Uingereza, Lithuania, Latvia na Estonia - jamhuri za zamani za Soviet zinazopakana na Urusi. Urusi inawaona wanajeshi wa Nato mashariki mwa Ulaya kama tishio la moja kwa moja kwa usalama wake.
Bw Putin amebishana kwa muda mrefu kuwa Marekani ilivunja hakikisho ililoweka mwaka 1990 kwamba Nato haitapanua kwenda mashariki zaidi, ingawa kuna utata juu ya kile kilichofikiwa.
Urusi ilimega rasi ya Crimea kusini mwa Ukraine mwaka 2014. Pia inawaunga mkono waasi walioteka maeneo makubwa ya eneo la mashariki la Donbas muda mfupi baadaye, na takriban watu 14,000 wameuawa kwenye mapigano katika eneo hilo.
CHANZO BBC SWAHILI
0 Comments