Na Witness Masalu,Mbeya.
Ikiwa ni maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa Kijinsia, imebainika kwamba mmomonyoko wa Maadili ni sababu kubwa inayochangia ukatili wa Kijinsia kuendelea Vyuoni hasa Rushwa ya Ngono.Hayo yamejitokeza katika mjadala uliofanyika kwenye Chuo cha Sayansi na Teknolojia mkoani Mbeya wakati msafara wa kupinga ukatili wa Kijinsia ukiendelea kutoa elimu katika maeneo mbalimbali nchini.
Akitoa maoni yake,mmoja wa wanafunzi wa chuo hicho Laurencia Petro alisema baadhi ya wanafunzi wamekua na tabia ya kuwashawishi wakufunzi wao kuwapatia alama kubwa kwa kutoa Rushwa ya ngono.
Laurencia amewaasa wanafunzi wenzake kujiheshimu ili kuepukana na muendelezo wa vitendo vya ukatili wa kijinsia.
“Kuvaa mavazi yenye maadili wanapoenda kuwaona walimu wao, kuongea kwa kujiamini na kuzingatia muda sahihi wa kuwaona walimu inaweza kuepusha uombwaji wa Rushwa ya ngono” alisema Laurencia.
Kwa upande wake mratibu wa dawati la jinsia Mkoa wa Mbeya Inspekta Loveness Mtemi amedai kwamba amekuwa akipokea taarifa za wanafunzi kufanyiana ukatili wa kijinsia wao wenyewe wakiwa Vyuoni juu ya sababu mbalimbali hususani mahusiano ya Mapenzi na kuwasisitiza waache hiyo tabia.
“Kuna ukatili wa Kisaikolojia kwa asilimia kubwa, utakuta mwanaume anampa mwanamke maneno magumu yanayodhoofisha na mwisho kuishia kupata magonjwa ya Sukari na Presha.”
Aliwaasa pia wanawake kuacha kuwapa wenzi wao maneno magumu kama ‘wanaume suruali’, hivyo kuishia kupata Sonona na mwisho wa siku masomo kushindikana.
Akizungumza katika mjadala huo, Afisa Maendeleo ya Jamii kitoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Staricko Meshack amewaasa wanafunzi kubadilika wao wenyewe na kukemea vitendo hivyo, kuelimishana na kutoa taarifa mara moja wanapoona kuna viashiria vya rushwa.
0 Comments