SUAMEDIA

Tanzania yatoa ufafanuzi juu ya mtu aliyeripotiwa kuwa na Omicron

 Wizara ya Afya nchini Tanzania imetoa ufafanuzi juu ya abiria aliyeripotiwa kuwa na anuai mpya ya uviko 19 nchini India kuwa ametokea Tanzania.



Wizara imesema imepokea taarifa iliyoripotiwa na vyombo vya habari vya India na kuenea katika mitandao ya kijamii ikieleza kuwa India wamegundua abiria mmoja anayerudi nyumbani (India) mwenye anuai mpya ya Omicron ambaye ametokea Tanzania.

Hata hivyo haijajulikana kama abiria huyu alitokea Tanzania moja kwa moja au alipita Tanzania kuelekea India. Pia haijajulikana alipita wapi kabla ya kufika India.

Kutokana na taarifa hizo, Wizara ya Afya imeanza kufuatilia kupitia vyombo vyetu vya ndani na pia kwa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania nchini India ili kubaini ukweli wa jambo hili na baadae kuchukua hatua stahili.

Aidha wizara imetaka wananchi kutokuwa na hofu kutokana na habari hii, bali tuendelee kuwa watulivu na kutekeleza shughuli za maendeleo huku tukichukua tahadhari zote; ikiwa ni pamoja na kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka, kuvaa barakoa, kujiepusha na misongamano isiyokuwa ya lazima na kufuata miongozo mbalimbali inayotolewa na Wizara katika kupambana na UVIKO-19.

CHANZO BBC SWAHILI

Post a Comment

0 Comments