SUAMEDIA

Marekani yatoa Dozi nyingine Milioni 1.6 Za Chanjo dhidi ya Uviko-19 kwa Tanzania

 


 Tanzania jana imepokea shehena nyingine ya zaidi ya dozi milioni 1.6 ya chanjo dhidi ya UVIKO-19 aina ya Pfizer BioNTech zilizotolewa na Serikali ya Marekani kupitia Mpango wa Kimataifa wa Usambazaji chanjo wa COVAX.

 Msaada huo ulipokelewa rasmi na Kaimu Meneja wa Programu ya Kinga na Chanjo kutoka Wizara ya Afya Dk. Ngegwe Bulula, kutoka kwa Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) nchini Tanzania, Kate Somvongsiri, katika hafla fupi iliyofanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.

Kama sehemu ya jitihada zake za kulitokomeza janga hili duniani kote, hadi hivi sasa Serikali ya Marekani imeipatia Tanzania zaidi ya dozi milioni 3 za chanjo dhidi ya UVIKO 19.  Shehena ya kwanza kutoka Marekani iliyohusisha zaidi ya dozi milioni 1 za aina ya Johnson and Johnson ilipokelewa mwezi Julai na hivyo kuiwezesha Tanzania kuzindua kampeni ya kitaifa ya chanjo dhidi ya virusi vinavyosababisha UVIKO-19. 

Mwezi Novemba, Serikali ya Marekani ilitoa dozi 500,000 za chanjo aina ya Pfizer BioNTech ili kusaidia zaidi jitihada za Tanzania za kukabiliana na kusambaa kwa UVIKO-19. Jitihada hizi ni kielelezo cha ubia imara na dhamira ya dhati ya Serikali ya Marekani kwa watu wa Tanzania na malengo yetu ya pamoja ya kuushinda UVIKO-19 kwa pamoja.

“Tumedhamiria kwa dhati kuisaidia Tanzania na dunia kushinda vita dhidi ya UVIKO-19. Tunaipongeza Serikali ya Tanzania kwa jitihada zake za kuwachanja watu wake na tunatumaini mchango huu wa ziada wa chanjo utawezesha kuongezwa kasi ya kampeni ya chanjo na kutupeleka karibu zaidi na kulimaliza janga hili,” alisema Balozi wa Marekani nchini Tanzania Donald Wright.

Msaada wa Marekani katika jitihada za kimataifa za kukabiliana na UVIKO-19 unajumuisha:

    Kuchangia dozi milioni 300 za chanjo kwa nchi nyingine.
    Kununua dozi bilioni 1 za chanjo na kuzitoa kwa takriban nchi 100 zinazoendelea.
    Kuchangia Dola za Kimarekani bilioni 4 kusaidia Mpango wa Kimataifa wa Usambazaji Chanjo COVAX, unaolenga kusambaza chanjo dhidi ya UVIKO-19 duniani kwa usawa na ufanisi.
    Kusambaza dawa muhimu na vifaa tiba pamoja na kuzisaidia nchi kujenga upya uchumi wao, kukabiliana na upungufu wa chakula na kuimarisha usalama wa afya.

Hadi hivi sasa Marekani imeshatoa zaidi ya dozi milioni 80 ya chanjo dhidi ya UVIKO -19 na zaidi ya Dola za Kimarekani bilioni1.9 kama msaada unaohusiana na UVIKO-19 bila masharti yoyote.

Rais wa Marekani Joe Biden ameahidi kuwa Marekani itakuwa ghala la dunia la chanjo dhidi ya UVIKO-19 katika mapambano ya pamoja dhidi ya janga hili. “Tutaendelea kufanya kila linalowezekana kuifanya dunia kuwa mahali salama zaidi dhidi ya kitisho cha magonjwa ya kuambukiza,” Alisema Rais Biden mwanzoni mwa mwaka huu.

Post a Comment

0 Comments