Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango leo desemba 6, 2021 amefungua kikao cha awali cha nchi wanachama wa Umoja wa Afrika cha Jukwaa la Kujadili Masuala ya Usawa wa Kijinsia kikao kilichofanyika kwa njia ya mtandao. Kikao hicho kinachagizwa na kauli mbiu isemayo “Kuimarisha upatikanaji wa fursa kwa wanawake katika uongozi na nafasi za maamuzi ili kufikia ajenda ya Afrika tunayoitaka”.
Aidha ameongeza kwamba ili kufikia ajenda ya “Afrika Tuitakayo” bara la Afrika linahitaji usawa katika uongozi, uwakilishi sawa katika masuala ya siasa pamoja na mazingira ya usawa katika masuala ya kijamii na kiuchumi.
Makamu wa Rais amesema serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua kwamba usawa wa kijinsia pamoja na uwezeshaji wanawake kiuchumi ni nguzo muhimu katika kufikia maendeleo endelevu kwa jamii yeyote ile ndio maana serikali imekua ikiingia katika mikataba ya kitaifa, kikanda na kimataifa inayohusu kuimarisha usawa wa kijinsia, kuwawezesha wanawake kiuchumi pamoja na kuimarisha uwezo wa wanawake katika uongozi na nafasi za maamuzi katika sekta zote za maendeleo.
Amesema Tanzania inaendelea kutekeleza ahadi zake ilizotoa katika Jukwaa la Kizazi Chenye Usawa (Generation Equality Forum) ambazo zililenga kukuza na kulinda haki za kiuchumi kwa wanawake.
Ameongeza kwamba kwa kutambua Elimu ndio msingi utakaowezesha kufikia malengo ya ushiriki sawa wa wanawake katika masuala ya kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni ikiwemo kuwawezesha wanawake kushiriki katika uongozi, serikali ya Tanzania tangu mwaka 2016 ilianzisha sera ya elimu bila malipo kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha nne pamoja na kuhimiza wasichana kusoma masomo ya sayansi kwa kuweka miundombinu itakayowawezesha ikiwemo ujenzi wa shule za sayansi maalum kwa wasichana katika kila mkoa.
Pia Makamu wa Rais amesema serikali imeondoa vikwazo vya umiliki wa ardhi kwa wanawake nchini Tanzania pamoja kuwawezesha kupata mikopo kutoka katika asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri ili kuwawezesha kiuchumi.
Makamu wa Rais amesema ni muhimu nchi za Afrika kuendelea kuchukua hatua katika kuweka sera na sheria rafiki pamoja na kuwasihi viongozi wa Afrika kuweka mikakati itakayowezesha kutatua changamoto zote zinazokwamisha ushiriki wa wanawake katika uongozi na nafasi za maamuzi.
Ufunguzi wa kikao hicho cha awali umehudhuriwa na Viongozi wa Juu kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika , Wawakilishi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa pamoja na mashirika yasio ya serikali. Kikao hicho ni maandalizi ya mkutano mkuu wa viongozi wakuu wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) unaotarajiwa kufanyika Februari 2022.
0 Comments