SUAMEDIA

WAZIRI MCHENGERA AELEKEZA MCHAKATO WA AJIRA ZOTE SERIKALINI URATIBIWE NA SEKRETARIETI YA AJIRA ILI KUTENDA HAKI

 

Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa ameelekeza mchakato wa ajira katika taasisi zote za umma nchini uratibiwe na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kama chombo huru ili kuleta uwazi na kuwezesha haki kutendeka.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akiteta jambo na Naibu Waziri wake, Mhe. Deogratius Ndejembi kabla ya Mhe. Mchengerwa kuzindua Bodi ya Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma leo jijini Dodoma.

Mhe. Mchengerwa ametoa maelekezo hayo leo jijini Dodoma wakati akizindua Bodi ya Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma iliyopewa dhamana ya kusimamia mchakato wa ajira katika Utumishi wa Umma.

Mhe. Mchengerwa amesema amelazimika kutoa maelekezo hayo kwasababu hivi karibuni baadhi ya waajiri wamekuwa wakiomba vibali vya ajira na kutaka kuendesha mchakato wa ajira wao wenyewe katika taasisi zao hali inayoondoa uwazi, ushindani na usawa katika kuendesha mchakato wa ajira.

Amesema lengo la Serikali ni kuondoa upendeleo unaotokana na undugu, ukabila, udini na masuala mengine yasiyo ya kimaadili katika mchakato wa ajira kwenye Utumishi wa Umma.

“Utakuta baadhi ya taasisi, watumishi wake wameajiriwa kindugu, kidini na kikabila, nikiwa ndiye Waziri mwenye dhamana ya kusimamia utendaji kazi wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, ninataka tuondokane na changamoto hiyo ili twende kwenye uwazi na haki katika mchakato wa ajira Serikalini kama ambavyo Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ameelekeza,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.

Mhe. Mchengerwa amesema baada ya maelekezo aliyoyatoa, hategemei kusikia taasisi yoyote ya umma inafanya mchakato wa ajira bila kupitia Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.

Aidha, Mhe. Mchengerwa amewataka Wajumbe wa Bodi aliyoizindua, kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia weledi kwani wameaminiwa na Serikali na ndio maana wakapewa nafasi hizo ili kuisaidia Serikali kupata watumishi wenye uwezo ambao watatoa mchango kwa maendeleo ya taifa.

Akitoa neno la Shukrani, Mwenyekiti wa Bodi ya Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Bibi Sophia Kaduma amemshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumteua kuwa Mwenyekiti wa Bodi hiyo na Mhe. Mchengerwa kwa kuwateua Wajumbe wa Bodi yake.

Bibi Kaduma amemhakikishia Mhe. Mchengerwa kuwa wanao uwezo wa kutekeleza majukumu waliyopewa kwa ufanisi na kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za mchakato wa ajira ili Serikali iweze kupata watumishi watakaoweza kuleta maendeleo katika taifa.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ofisi yake, Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Bw. Xavier Daudi, amesema ofisi yake imefanya maboresho ya utendaji kupitia TEHAMA inayowezesha kutoa taarifa za ajira kupitia tovuti (www.ajira.go.tz) tofauti na awali ambapo walilazimika kutangaza ajira kupitia vyombo vya habari.

Bw. Daudi amesema, tovuti hiyo inatumika kutoa matangazo ya ajira na ufafanuzi wa masuala mbalimbali yanayohusina na ajira. 

Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, ilianzishwa kwa mujibu wa Kifungu 29(1) cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298 (iliyorejewa 2019) kwa ajili ya kushughulikia mchakato wa ajira katika Utumishi wa Umma.

Wajumbe wa Bodi ya Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma na baadhi ya watendaji wa Sekretarieti wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa wakati akizindua bodi hiyo leo jijini Dodoma.

Katibu wa Sekretarieti ya Ajira Katika Utumishi wa Umma, Bw. Xavier Daudi akielezea majukumu ya ofisi yake kabla ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa kuzindua Bodi ya Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma leo jijini Dodoma.

Mwenyekiti wa Bodi ya Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Bibi Sophia Kaduma akitoa neno la shukrani kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa kwa kuzindua bodi hiyo leo jijini Dodoma.






Post a Comment

0 Comments