Na Gerald Lwomile, Rungwe, Mbeya.
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeuomba uongozi wa
Halmashauri ya Rungwe mkoani Mbeya kuhakikisha unazingatia mapendekezo
yaliyotolewa katika mkutano wa kisera ili kuhakikisha kunakuwa na ongezeko la
uzalishaji wa malisho ya wanyama wilayani humo.
 |
| Prof Chove akikabidhi nyaraka mbalimbali kwa mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Rungwe Bw. Augustino Lawi |
Ombi hilo limetolewa Novemba 12, 2021 na Makamu wa Mkuu wa
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael Chibunda katika hotuba
iliyosomwa kwa niaba yake na Prof. Bernard Chove ambaye pia ni Rasi wa Ndaki ya
Kilimo SUA wakati wa Makabidhiana ya Kituo cha Maarifa Ilenge kilichokuwa chini
ya Mradi wa InnovAfrica.
Akisoma hotuba hiyo Prof. Chove amesema katika mkutano wa
kisera uliokutanisha wadau mbalimbali zilibainika changamoto kadhaa
zinazokabili uzalishaji wa malisho bora ya mifugo ikiwa ni pamoja na
upatikanaji wa mbegu bora za malisho, uhitaji wa taarifa za ufugaji bora na
wafugaji wengi hawajafikiwa na huduma ya uzalishaji wa malisho.
“Kwanza Serikali kupitia huduma za ugani iongeze uelewa wa
wafugaji kuhusu malisho haya kwa kutumia shamba mfano na hivyo kuongeza uhitaji
wa malisho hayo……., pia wakulima wa mfano watumike kama huduma za ugani ili
kuendeleza uzalishaji wa malisho aina ya Bracharia” alisema Prof. Chove
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya
Rungwe wakati wa kupokea Kituo hicho cha Maarifa Ilenge Afisa Mifugo na Uvuvi
wa wilaya hiyo Bw. Agustino Lawi amesema utafiti wa malisho uliofanywa na Mradi
wa InnovAfrica chini ya SUA umeleta mafanikio makubwa katika wilaya hiyo ikiwa
ni pamoja na uzalishaji wa maziwa kuongezeka lakini pia maziwa yake sasa yana
ubora unaokidhi viwango bora vya maziwa
“Ulishaji wa migomba ambao umezoeleka sana katika maeneo yetu
mara nyingi umekuwa na matokeo mabaya, kwani unatoa maziwa mepesi na maziwa
mepesi hayakubaliki katika soko, kwa hiyo niombe tuendelee kuzalishaji malisho
na tuna nafasi ya kuboresha lishe” amesema Bw. Lawi
Nao wafugaji na wakulima wa mfano katika mradi huo Bw. Kayusi
Msigwa na Bibi Tumaini Sigile wamesema kumekuwa na manufaa makubwa katika
kilimo cha malisho aina ya Bracharia pamoja na kuwepo kwa changamoto kadhaa
ikiwa ni pamoja na malisho hayo kutofanya vizuri katika kipindi cha kiangazi
ambapo hata hivyo walishauriwa kufanya umwagiliaji katika kipindi hicho
Awali akitoa tathimini ya mradi huo Mkuu wa Mradi huo ambao
tayari umekabidhiwa kwa Halmashauri ya Rungwe Prof. Dismas Mwaseba amesema
katika utafiti wao wameona malisho aina ya Brachiaria Basilisk ndiyo yamefanya
vizuri zaidi katika wilaya ya Rungwe
Mradi wa InnovAfrica umeendeshwa kwa miaka 3 katika wilaya
mbili hapa nchini ambazo ni Lindi na Rungwe na kwa upande wa Rungwe mradi huo
uliofadhiliwa na Jumuiya ya Ulaya ulilenga kuhakikisha Usalama wa Chakula kwa
kuboresha malisho kwa ngombe wa maziwa na kuanzisha Kituo cha Maarifa cha
Kijiji ambacho kinaweza kuwasaidia wakulima na wafugaji kujipatia taarifa
mbalimbali za kitaalamu
 |
| Mwakilishi wa Makamu Mkuu wa Chuo na Rasi wa Ndaki ya Kilimo SUA Prof. Chove katikatii aliyevaa tai akiwa katika picha ya pamoja na wadau mbalimbali walioshiriki katika makabidhiana hayo kulia kwa Prof, Chove ni Mkuu wa Mradi huo uliomaliza muda wake Prof. Dismas Mwaseba |
0 Comments