SUAMEDIA

Mhe. Innocent Bashungwa aagiza Halmashauri za Wilaya, Miji na Jiji kutenga bajeti ya ujenzi wa Miundombinu ya Michezo

 

Na.Vedasto George

 Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mh. Innocent Bashungwa ameziagiza Halmashauri za wilaya, miji na majiji kuendelea kutenga bajeti kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya michezo katika maeneo yao hatua itakayosaidia kujiongezea mapato na kuamsha hali ya ushiriki wa michezo kwa watumishi wa umma .

 




Akizungumza wakati wa kuhitimisha michezo ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali Tanzania (SHIMIWI) mjini Morogoro Mh. Bashungwa amesema kuwa halmashauri za wilaya,miji na majiji ni vyema zikajenga miundombinu ya michezo kwenye maeneo yao ili kutoa fursa ya michezo kufanyika kwao na kuweza kuwafanya watumishi kushiriki katika michezo kwa wingi.

 

”Ndugu viongozi mlioko hapa  nitoe wito kwa Halmashauri za wilaya, miji na majiji  yetu kote nchini kuendelea kujenga miundombinu ya michezo katika maeneo yao hii itatusaidia sisi serikali kuwa na watumishi wapenda michezo, watumishi walio na afya lakini watumishi watakao weza kushindana pale yanapatokea mashindano ya kimichezo”, alisema Mh. Bashungwa.

 

Katika hatua nyingine waziri Bashungwa  ameliagiza Baraza la Michezo la Taifa BMT  kuhakikisha wanasimamia vyema  uchaguzi wa viongozi wa SHIMIWI utakaofanyika mwaka huu ili  kuweza kupata viongozi imara wataokaoweza kuliendesha na kufuata misingi ya  Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali Tanzania huku akisisitiza kuwa chaguzi nyingi za vyama vya michezo na mashirikisho yamekuwa yakikubwa na figisufigisu jambo ambalo linahatarisha ustawi wa michezo nchini.

 

Kwaupande wake mwenyekiti wa SHIMIWI Taifa Daniel Mwalusamba ameiomba serikali kupitia wizara husika ya michezo kuangalia namna ya kuviendeleza vipaji vya watumishi wa umma ili kuwawezesha kuwa miongoni mwa wachezaji  watakao weza kulitumikia taifa kwa upande wa michezo

 

Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela amewashauri washiriki kutumia fursa hiyo waliyoipata wanaporejea kwenye maeneo yao ya kazi kwa kufanya kazi kwa ufanisi kujituma na kufuata misingi na maadili ya utumishi wa umma huku akiongeza kuwa michezo ni sehemu mojawapo ya kumkumbusha mtumishi kuwa bado analo jukumu la kuwatumikia wananchi .

 

Kwa mwaka huu mashindano hayo yameshirikisha wanamichezo  zaidi ya 1800 kutoka wizara 24, mikoa 11, wakala wa serikali 4 na idara nane za serikali na kushirikisha timu 47.

 

Mashindano hayo ya SHIMIWI ambayo ni ya 35 yamefanyika kwa  mara ya kwanza tangu yasimamishwe kutokana na serikali kujielekeza zaidi katika utekelezaji wa miradi huku kwa upande wa mkoa wa Morogoro yakifanyika kwa mara ya sita.

 

 

 


 

Post a Comment

0 Comments