Na: Gladness Mphuru
Balozi wa Marekani nchini Tanzania Donald J Wright, amesema Marekani itaendelea kuimarisha ushirikiano na Tanzania katika kuinua na kuimarisha sekta ya Kilimo kwa kushirikiana na Chuo kikuu cha Sokoine cha kilimo SUA, kwa kufanya tafiti, kutoa elimu na uvumbuzi.
Ameyasema hayo leo novemba 11, 2021 kwenye ukumbi wa SUA multipurpose, katika maadhimisho ya miaka 60 ya uhusiano wa kidiplomasia baina ya Tanzania na Marekani, akiambatana na Naibu makamu mkuu wa chuo kikuu cha Sokoine cha kilimo SUA utawala na fedha prof. Maulid Mwatawala akimuwakilisha Naibu makamu mkuu wa Chuo Prof. Raphael Chibunda, mkuu wa wilaya ya mvomero Mhe. Halima Okash kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Morogoro, pamoja na mkurugenzi mtendaji wa REPOA Dkt. Donald Mmari.
Balozi Wright amesema kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita serikali yake kupitia shirika la Marekani la maendeleo ya kimataifa USAID lilitumia dola milioni 200 kwenye mkakati wa feed the future, na ushirikiano baina ya nchi hizo mbili umeweza kuwanufaisha wakulima zaidi ya 700,000 na wazalishaji wengine wa chakula.
Aidha amesema kuwa juu ya mkakati wa Feed The Future, serikali yake imelenga kuchangia asilimia 20 kupunguza umasikini kwa Tanzania na nchi zingine lengwa kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, na kuongeza kuwa katika hatua hiyo Rais wa nchi hiyo Joe Biden ameidhinisha bajeti ya kiasi cha dola billion 5 ya mpango huo.
Awali akizungumza Naibu Makamu mkuu wa SUA utawala na Fedha Prof. Maulid Mwatawala, amesema ushirikiano baina Chuo kikuu cha SUA na serikali ya marekani umewezesha kwa kiasi kikubwa miradi mbalimbali pamoja na tafiti za kilimo chuoni hapo, hivyo kimeweza kuwasaidia wakulima wa Tanzania kukabiliana na changamoto za kilimo.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya mvomero Mhe. Halima Okash amesema serikali inahitaji kutumia wasomi kutoka SUA kutafuta utatuzi wa changamoto zinazowakumba wakulima wa Tanzania ikiwemo magonjwa ya mazao, wadudu shambulizi na mabadiliko ya Tabia nchi.
Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa shirika lisilo la kiserikali Research on poverty alleviation REPOT Dkt. Donald Mmari, amesema kupitia ushirikiano huo wasomi wengi watanzania wameweza kupata fursa ya kusoma nchini marekani na nchi zingine zilizoendelea, kuwa imesaidia kuendelea kuongeza kasi ya ukuaji kiuchumi nchini.








0 Comments