Rais wa Afrika Kusini amelaani marufuku ya kusafiri iliyowekwa dhidi ya nchi yake na majirani zake kutokana na aina mpya ya kirusi cha Corona Omicron.
Cyril Ramaphosa alisema "amesikitishwa sana" na hatua hiyo, ambayo aliitaja kuwa isiyo na msingi, na kutaka marufuku hiyo kuondolewa haraka.
Uingereza, EU na Marekani ni miongoni mwa walioweka marufuku ya kusafiri.
Omicron imeainishwa kama "aina ya kuhofisha ". Ushahidi wa mapema unaonyesha kuwa ina hatari kubwa ya kuambukizwa tena.
Kirusi hicho kinachobadilika kwa haraka sana kiligunduliwa nchini Afrika Kusini mapema mwezi huu na kisha kuripotiwa kwa Shirika la Afya Duniani (WHO) Jumatano iliyopita.
Aina hiyo inawajibikiaa maambukizi mengi yanayopatikana katika jimbo lenye wakazi wengi zaidi la Afrika Kusini, Gauteng, katika kipindi cha wiki mbili zilizopita, na sasa ipo katika majimbo mengine yote nchini.
WHO imeonya dhidi ya nchi zinazoweka vikwazo vya kusafiri kwa haraka, ikisema wanapaswa kuzingatia "mbinu ya hatari na ya kisayansi". Walakini, marufuku nyingi zimeanzishwa katika siku za hivi karibuni huku kukiwa na wasiwasi juu ya Omicron .
Mkurugenzi wa Afrika wa WHO Matshidiso Moeti alisema Jumapili: "Pamoja na aina hiyo ya Omicron sasa iliyogunduliwa katika maeneo kadhaa ya dunia, kuweka marufuku ya kusafiri ambayo inalenga Afrika inaathiri mshikamano wa kimataifa."
Katika hotuba yake siku ya Jumapili, Bw Ramaphosa alisema hakuna msingi wa kisayansi wa marufuku ya kusafiri na kwamba eneo la kusini mwa Afrika ndilo lililoathiriwa na ubaguzi usio wa haki.
Pia alidai kuwa marufuku hizo hazitakuwa na ufanisi katika kuzuia kuenea kwa aina hiyo hiyo.
"Kitu pekee ambacho katazo la kusafiri litafanya ni kuharibu zaidi uchumi wa nchi zilizoathirika na kudhoofisha uwezo wao wa kukabiliana na janga hili," alisema.
Alitoa wito kwa nchi zilizoweka marufuku "kubadilisha maamuzi yao haraka ... kabla ya uharibifu wowote kufanywa kwa uchumi wetu".
Bw Ramaphosa alielezea kuibuka kwa aina ya kirusi cha Omicron kama wito wa kuamsha ulimwengu kuhusu kukosekana kwa usawa wa chanjo - akionya kwamba hadi kila mtu apewe chanjo, aina nyingine zaidi haziwezi kuepukika.
Hakuna uhaba wa chanjo nchini Afrika Kusini kwenyewe, na Bw Ramaphosa alihimiza watu zaidi kuchanja, akisema hiyo inasalia kuwa njia bora ya kupambana na virusi.
Taarifa ya awali ya wizara ya mambo ya nje ya Afrika Kusini siku ya Jumamosi pia ilikosoa vikali marufuku ya kusafiri, ikisema nchi hiyo inaadhibiwa - badala ya kupongezwa - kwa kugundua Omicron.
Omicron sasa imegunduliwa katika nchi kadhaa duniani kote, ikiwa ni pamoja na Uingereza, Ujerumani, Australia na Israel.
Katika matukio mengine ya Jumapili:
• Nchini Uholanzi, Omicron iligunduliwa katika watu 13 waliofika Amsterdam kwa ndege mbili kutoka Afrika Kusini.
• Kwingineko, polisi wa Uholanzi walisema wamewazuilia wanandoa ambao walikuwa wametoroka kutoka kwa hoteli walimotengwa. Kukamatwa huko kulifanywa kwenye ndege muda mfupi kabla ya kupaa
• Israel ilipiga marufuku wageni wote kuingia nchini kwa siku 14 kuanzia saa sita usiku Jumapili
• Uingereza iliitisha mkutano wa dharura wa kundi la mataifa ya G7 siku ya Jumatatu kujadili aina hiyo mpya ya Corona
• Wapiga kura nchini Uswizi waliunga mkono hatua za serikali za kukabiliana na Covid, kulingana na matokeo ya awali
0 Comments