SUAMEDIA

SUA, PASS kusaidia vijana kujiajiri

 

Calvin Gwabara na Gladness Mfuru

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Jaji Mstaafu Mhe. Joseph Sinde Warioba amefurahishwa na mafunzo yanayotolewa na SUA kwa kushirikiana na PASS (Private Agricultural Support Sector) yanayosaidia vijana kujiajiri Mhe. Jaji Warioba ametoa pongezi hizo Octoba 25, 2021 wakati wa ziara yake ya siku mbili Chuoni hapo, akiwa ameambatana na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Jaji Othman Chande na Makamu Mwenyekiti wake Bi. Doroth Mwanyika.



“Hawa vijana wakitoka hapa watasaidia kuwa walimu kwa jamii inayowazunguka na tayari wana kitu cha kufanya ukweli nimefurahi sana kuona vijana kutoka Mikoa mbalimbali kama Tabora, Mwanza, Kigoma, Rukwa wakipata mafunzo haya” alisema Mhe. Jaji Warioba.

Jaji Warioba amesema mafunzo hayo yatalisaidia taifa kwa kiasi kikubwa katika miaka ijayo katika kukidhi mahitaji ya chakula na kuepukana na baa la njaa kutokana na ongezeko la watu “Wakati nchi inapata uhuru tulikuwa Watanzania milioni 9 lakini sasa wamefika milioni 60 hivyo tutarajie ongezeko kubwa la watu na uhitaji mkubwa wa chakula”.

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) amekitaka chuo hicho kuongeza elimu kwa upana ili kuwafikia vijana wengi zaidi kwani mafunzo hayo tayari yameshaleta mafanikio kwa jamii kupitia vijana waliopita ambao walipata mafunzo hayo.

Kwa upande wa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Prof. Raphael Chibunda amemshukuru Mkuu wa Chuo hicho kwa kazi kubwa aliyoifanya katika kipindi cha miaka minne na mafanikio yaliyopatikana.

Prof. Chibunda amesema kuwa wamefanya maboresho makubwa chuoni hapo kwa kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia kwa wanafunzi hususani mashamba kwa vitendo ikiwemo ujenzi wa Maabara na ununuzi wa vifaa vya kisasa vya maabara pamoja na ujenzi ikiwemo Maabara mtambuka ambayo inaweza kuchukua wanafunzi 3200 kwa wakati mmoja.

Makamu Mkuu wa Chuo amesema kuwa Chuo kimetenga fedha zaidi ya sh. milioni 450 kwa ajili ya kujenga vitalu 100 katika kipindi cha miaka mitatu, ambapo kwa mwaka huu wataanza na vitalu 30 na tayari wamepeleka maombi mahususi kwa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa lengo la kushirikiana kuendeleza wabunifu kwa kujenga vitalu vingi zaidi.

Aidha, ameongeza kuwa tayari milioni 200 zimetumika kwa ajili ya upanuzi wa sehemu ya upasuaji na manunuzi ya vifaa vipya kama mashine ya X- Ray Digital, Ultra Sound ya kisasa yenye kuwezesha kuona kama mnyama amepata tatizo kubwa zaidi kwa ndani lakini pia Chuo kipo mbioni kununua gari itakayotumika kama kliniki inayotembea ili kuwafikia wafugaji wanaoshindwa kufika kwenye Hospitali hiyo ya Taifa ya Rufaa ya Wanyama ili kupatiwa matibabu.

“Nitoe wito kwa wafugaji wa wanyama katika nchi hii pale wanapoona wamekosa msaada sehemu nyingine basi waitazame Hospitali yetu ya Rufaa ya Taifa ya Wanyama kama sehemu ya kupata msaada” amesema Profesa. Chibunda.

Katika ziara hiyo Jaji Mstaafu Mhe. Joseph Sinde Warioba ametembelea Ndaki mbalimbali ikiwemo Ndaki ya Tiba ya Wanyama na Sayansi za Afya, Ndaki ya Kilimo kwenye Shamba la mafunzo, Maabara mtambuka, Kituo atamizi cha Vijana kilichopo chini ya Shule kuu ya Uchumi Kilimo na taaluma za biashara, Kitengo cha Mifugo Magadu, Kitengo cha Samaki Magadu na Maabara ya Sayansi na Teknolojia ya chakula.

KATIKA VIDEO

https://youtu.be/EhCO5voCQfg

Post a Comment

0 Comments