SUAMEDIA

SUA imeendelea kuunga mkono Sera za Nchi na mwelekeo wa Taifa kuelekea kukuza Uchumi wa viwanda

 

Na.Vedasto George.                                       

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kimeendelea na jitihada zake za kuunga mkono  sera za nchi na mwelekeo wa taifa kuelekea kukuza uchumi wa viwanda kwa kuhakikisha  kinatoa wataalam wenye ujuzi na maarifa ambayo yatasaidia katika kuinua uchumi wa viwanda vidogo na vya kati ambavyo vimenzishwa  nchini.


Mratibu wa Utafiti na Machapisho SUA Prof. Japhet Kashaigili akifungua Mafunzo ya Kongano la Nguo  mjini Morogoro yaliyoratibiwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Morogoro.


Hayo yamebainishwa na Prof. Japhet Kashaigili ambaye ni Mratibu wa Utafiti na Machapisho SUA wakati akifungua Mafunzo ya Kongano la Nguo  mjini Morogoro yaliyoratibiwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA  kupitia kitengo cha Sayansi ya Mraji yaliyowajumuisha Mafundi nguo na Wabunifu wa mavazi kwa mkoa wa Morogoro.

"Kituo cha Ubunifu kilichopo katika Kurugenzi hii kimejikita katika kutoa elimu ya bunifu  mbalimbali, hati miliki, tafiti, uhaulishaji wa Teknolojia kwa wanafunzi., watafiti na   wajasiriamali wa viwanda  vidogo na vya kati na dhumuni kubwa la kituo hiki ni kutoa maarifa shirikishi , kuchochea ubunifu kwa kuunganisha  watu wenye fikra na mtazamo sawa  ndani na nje ya Chuo cha Sokoine cha Kilimo, lakini Kwa ujumla kituo hiki kinalenga kujenga bunifu na ujasiriamali kwa kuboresha mahusiano kati ya chuo, viwanda na taasisi nyingine za nje, "alifafanua Prof.Kashaigili.

Prof. Kashaigili ameongeza kuwa kitengo cha bunifu kilichoko  katika Kurugenzi  kitengo cha Sayansi ya Familia na Walaji  kilichoko Ndaki ya Kilimo,  kinalenga kuboresha bunifu, ujuzi, maarifa na tafiti zinazosaidia watu kufanya maamuzi yanayolenga ustawi, mahusiano,  na rasilimali ili kuweza kufikia  maisha bora zaidi.

Aidha Prof. Kashaigili amesema kitengo cha Sayansi ya Familia na Walaji kinajikita katika maeneo mengi ikiwa ni pamoja na ubunifu na ushonaji mavazi, mpangilio na upambaji wa ndani ya nyumba pamoja na masuala yanayohusisha sayansi ya walaji.

"Mafanikio  ya viwanda hivi  ikiwemo viwanda vya KONGUMO yanategemea namna  viwanda hivi  vinavyoweza  kuboresha teknolojia na kujenga uwezo na hatimaye kuzalisha aina nyingi zaidi za bidhaa za kuuza ndani na nje ya nchi hivyo kuongeza tija na faida kwa kutumia kiasi kidogo cha mtaji ", alisema  Prof.Kashaigili.

Kwa upande wake Mary Masere Mhadhiri na Mbobezi wa masuala ya Ubunifu wa Mavazi, Utengenezaji wa Samani na Mapambo ya ndani kutoka SUA amesema kutokana na mchango mkubwa unaotolewa na mafundi nguo nchni katika utengenezaji wa mavazi, Chuo kupitia washirika wake  kimeona kuna haja ya kuwaongezea ujuzi katika kazi yao ya ubunifu wa mavazi ili iweze kuwa na thamani zaidi.

"Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo zamani kilikuwa kinajulikana kinahusika na kilimo tu lakini hivi karibuni kuanzia mwaka 2010 chuo kiliweza kujipambanua na kwenda kwenye Nyanja nyingine ambazo zinamuhusu zaidi mlaji, sasa kupitia Kitendo  cha Sayansi ya Mlaji wakajiweka zaidi kwenye ubunifu wa mavazi tukitambua mavazi ni kitu muhimu kwa binadamu na tukasema isiwe tu bora mavazi lakini lazima vazi liwe la ubunifu ili mtu anapovaa muonekano wake uendane, kwa hiyo kupitia kitengo hiki cha ubunifu tukatambua kuwa kuna mafundi ambao wanasaidia kushona haya mavazi ndio maana leo tunawapa mafunzo",alisema Mary Masere.

Naye Robert Joseph Mwenyekiti wa  KONGUMO la nguo Manispaa ya Morogoro akizungumza kwa niaba ya washiriki wengine  amesema matarajio yao baada ya mafunzo ni kukakikisha wanafanya ubunifu wa mavazi  wenye tija na wenye kulenga soko la ndani na nje ya nchi huku akiongeza kuwa mafunzo hayo yatawabadilisha mafundi katika kutekeleza kazi zao na kuongeza uaminifu kwa wateja.



Post a Comment

0 Comments