Na. Nasra H. Mondwe-Arusha
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka Watunza Kumbukumbu na Nyaraka katika taasisi za umma kutekeleza majukumu yao kwa weledi ili kujiepusha na uvujishaji wa siri za serikali.
Mhe. Mchengerwa ametoa wito huo wakati akifungua Mkutano wa 9 wa Chama cha Taaluma ya Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania katika ukumbi wa ACC jijini Arusha.
Mhe. Mchengerwa amesema, dhamana waliyonayo Watunza Kumbukumbu ni kubwa, hivyo ni vema wakazingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za utunzaji wa kumbukumbu pamoja na viapo vyao kwasababu utoaji wa siri za Serikali ni kosa kubwa kisheria na kwa mujibu wa taratibu za Utumishi wa Umma.
Waziri Mchengerwa amewaasa washiriki wa Mkutano huo kuhakikisha wanajiepusha na siasa na mambo mengine yanayosababisha kutoa siri za Serikali.
Mhe. Mchengerwa amesisitiza kuwa, Serikali ya Awamu Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan inathamini mchango wa Watumishi wa Umma na itaendelea kulinda maslahi yao ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili Watunza Kumbukumbu, hivyo hakuna sababu ya watumishi kutoa siri za Serikali na badala yake wanapaswa kuwa waadilifu kiutendaji na kuwa watiifu kwa Serikali yao.
Akizungumzia juu ya stahiki mbalimbali za Watumishi wa Umma, Mhe Mchengerwa amewaagiza waajiri wote kuhakikisha wanalipa stahili zote za watumishi ikiwepo madai ya malimbikizo ya mishahara na kuongeza kuwa wanapaswa kutenga muda wa kusikiliza kero za watumishi na
kuzitafutia uvumbuzi.
Mhe. Mchengerwa amewasisitiza waajiri kuheshimu kada zote kwani kila kada ina umuhimu wake katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku ya Serikali.
“Waajiri ziheshimuni kada zote, msidharau kada za watu wa chini kwani hawa ni watu muhimu katika utekelezaji wa majukumu yetu na sisi kama Serikali tutaendelea kuzipigania kada hizi,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.
Akimkaribisha Mhe. Mchengerwa kufungua mkutano huo, Mwenyekiti wa Chama cha Taaluma ya Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA), Bi. Josephine Manase amesema lengo la chama chao ni kujengeana uwezo na kupeana hamasa ya utekelezaji wa majukumu kwa ufanisi ili kutoa mchango katika utekelezaji wa majukumu ya Serikali ya kila siku.
Aidha, Bi. Manase amemuomba Mhe. Mchengerwa kwa nafasi ya uongozi aliyonayo kukisaidia chama chake kumuomba Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Mgeni Rasmi katika Mkutano ujao wa 10 wa
Chama cha Taaluma ya Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania utakaofanyika Zanzibar, ikizingatiwa kuwa kazi ya kwanza ya Mhe. Rais ilikuwa ni ya utunzaji wa kumbukumbu Serikalini.
Mkutano huo wa siku tatu unaongozwa na kauli mbiu isemayo “Imarisha Utunzaji wa Kumbukumbu na Nyaraka ili kuwezesha Uwazi, Uwajibikaji na Utawala Bora katika Kutoa Huduma kwa Umma.”
0 Comments