Na; Calvin Gwabara - Kilosa
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro Alhaji Majid Hemed
Mwanga amesema wilaya yake haitamvumilia wala kumfumbia macho kiongozi au mwananchi
yeyote atakayecheza na rasilimali za Misitu kwa kufanya kinyume na utaratibu
uliowekwa kwenye vijiji vilivyo chini ya mpango wa usimamizi shirikishi wa Misitu
ya Vijiji na vile ambavyo bado havijaingia kwenye mpango huo.
Alhaji Mwanga ametoa kauli hiyo wakati wa ziara aliyoifanya akiwa
na Kamati ya Ulinzi na Usalama,Madiwani pamoja na viongozi wa Mashirika ya TFCG
na MJUMITA katika Kijiji cha Kitunduweta wilayani humo ili kujionea namna
mashirika hayo yanavyotekeleza Mpango simamizi shirikishi wa misitu kwenye
vijiji 20 vya Wilaya hiyo na kusikia shuhuda na mafanikio na kazi kubwa
zilizofanywa na mashirika hayo katika kufikia mafanikio hayo.
”Kwa kweli kazi kubwa sana imefanywa na wadau wetu Shirika la Kuhifadhi
Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) na Mtandao wa Jamii Usimamizi wa Misitu
Tanzania (MJUMITA) na sasa kazi iliyobaki ni sisi kuhakikisha elimu tuliyoipata
inaendelea kuleta matokeo chanya katika kutunza misitu yetu, na niseme tu
kwamba fedha nyingi mnapata kwenye vijiji lakini naomba mtambue kuwa fedha hizo
ni fedha za Umma zitumike kwa kufuata taratibu zote za matumizi ya fedha za
Umma na sio vinginevyo maana nina taarifa kuwa baadhi ya viongozi wanatumia
fedha hizo vibaya na kuna vijiji kamati zake kama Kijiji cha Ihombwe imeivunja”,alisisitiza
Alhaji Mwanga.
Mkuu huyo wa Wilaya aliwataka Wananchi kwenye vijiji hivyo
kutowafumbia macho viongozi wanaovuruga utaratibu mzuri ulioanzishwa bali watoe
taarifa kwenye ofisi yake na mamlaka zingine ili washughulikiwe na kuwasisitiza
kuendelea kuhifadhi misitu hiyo ya vijiji na kuitumia kwa uendelevu na kwa
maslahi mapana ya vijiji na Taifa.
“Ninyi sasa ni Walimu maana tumeona wenzenu kutoka kwenye
Wilaya ya Ruangwa anakotoka Mhe. Waziri Mkuu wetu walikuja kujifunza kutoka
kwenye Kijiji chenu sasa tuache kulalamika na kuendelea kulilia mafunzo zaidi
maana tunataka sasa hawa wadau wahamie kwenye vijiji vingine kwenye wilaya yetu
na mikoa mingine ili elimu hii ifike nchi nzima, tunachotaka sasa ni kuona
nyinyi mnasonga mbele kama walimu”, aliongeza Mkuu huyo wa wilaya ya Kilosa.
Alhaji Mwanga amewataka
wananchi kuacha kusikiliza maneno ya baadhi ya watu wanaokuja kuharibu misitu
na kuharibu taratibu zilizowekwa wakisingizia kuwa ni maagizo kutoka kwa
wakubwa na kuwataka waache kuwasiliza maana hamna maagizo yoyote yanayotoka juu
kwenye kuharibu misitu na akitokea mtu huyo watoe taarifa haraka ili watu hao
wakamatwe na kuchukuliwa hatua.
Mkuu huyo wa Wilaya ya Kilosa amewasisitiza viongozi wa Kijiji
na kamati za maliasili kila mmoja kutambua majukumu yake na kuacha kuingiliana
kwenye majukumu ili kuondoa migogoro isiyo ya lazima ambayo inatokana na hela
wanazozipata kutokana na mapata yanayokusanywa kwenye tozo na fedha za misitu.
Akieleza malengo ya Mradi huo
Meneja wa Mradi wa Mkaa endelevu Bw. Charles Lyimo amesema
lengo kuu ni kuhifadhi Misitu ya vijiji kikamilifu kutokana na tafiti kuonesha
kuwa kwa mwaka Tanzania inapoteza hekta 460,000 za misitu kutokana na shughuli
mbalimbali za uchomaji Mkaa, Kuni,Kilimo na Mbao na kiasi kikubwa cha upotevu
huo kinafanyika kwenye ardhi za vijiji katika maeneo ambayo hayajahifadhiwa.
Ameongeza kuwa katika kufanikisha hilo Mradi unawezesha vijiji
pamoja na Wilaya kuweza kuziwekea mpango bora wa kusimamia rasilimali hizo za
misitu vizuri ili kunufaika nazo kama vijiji lakini pia Serikali kwa ujumla.
Meneja huyo wa Mradi amesema lengo la pili ni kuchangia kwenye
maendeleo ya Wananchi maana hiyo ndiyo sera ya Serikali kwamba wananchi
wanaoishi pembeni mwa rasilimali za misitu waweze kunufaika nazo kwa njia
endelevu na hii ni katika kuwaonesha wananchi kuona rasilimali hiyo ya misitu
ni yao na wana jukumu la kuilinda na kuihifadhi kwakuwa wanapata motisha.
”Kupitia Program hii ya uhifadhi shirikishi wa misitu tunaona
kwamba kuna haja ya kuzidi kuiendeleza na jukumu kubwa tulilonalo hasa katika
awamu hii ya tatu ya mradi huu tayari tumeshaanza kuondoka kwenye vijiji vya
awali na wilaya ya Kilosa sasa tunahamia kwenye wilaya zingine nje ya mkoa wa
Morogoro na tumewaachia halmashauri ya Wilaya ili waweze kuwasimamia na
kuratibu hivi vijiji”, Alibainisha meneja wa Mradi.
Kwa upande wake Katibu wa Kamati ya Maliasili ya Kijiji cha
Kitunduweta, Leoti Msoloka amesema kupitia Usimamizi shirikishi wa Misitu ya
Kijiji chao wamepata mafanikio makubwa ikiwemo ujenzi wa Ofisi ya Kijiji,
Ukatabati wa vyumba vya madarasa,Ujenzi wa matundu ya vyoo pamoja na kuwakatia
bima ya afya iliyoboreshwa Wanakijiji wote kijijini hapo ambapo sasa wameanza
na ujenzi wa Zahanati ya Kijiji ili wapate huduma kijijini kwao.
“Faida kubwa ni kwamba hapo awali tulikuwa hatujui umuhimu wa
kuhifadhi Msitu wa Kijiji lakini baada ya elimu na faida tulizozipata na sasa
asilimia tisini ya mapato yatokanayo na misitu zinatumika kijijini tofauti na hapo
awali ambapo asilimia hizo zilikuwa zinaenda wilayani na sasa tunaweza
kuzitumia fedha hizo kulinda msitu na kunufaisha Kijiji chetu”,alifafanua Bw. Msoloka.
Mradi huu wa Uhifadhi Shirikishi wa Misitu ya Vijiji
unatekelezwa na Shirika la Kuhifadhi Misitu ya asili Tanzania (TFCG) na Mtandao
wa Jamii Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA) kwa ufadhili wa Shirika la
Maendeleo la USWISI (SDC).
0 Comments