SUAMEDIA

Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeahidi kuendelea kushirikiana na SUA katika kuendeleza Tafiti na Teknolojia za kisasa

 Na: Farida Mkongwe

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeahidi kuendelea kushirikiana na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA katika kuhakikisha Chuo hicho kinaendelea kufanya tafiti na kutengeneza teknolojia za kisasa za bei nafuu na zinazoweza kutumika kiurahisi ili kuinua sekta ya kilimo nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mh. Mashimba Ndaki wakati akifungua wiki ya kumbukizi ya Hayati Edward Moringe Sokoine inayofanyika katika Kampasi ya Edward Moringe iliyopo SUA Manispaa ya Morogoro kuanzia Mei 24 hadi Mei 27 mwaka huu.

Mh. Mashimba amesema wakulima wengi hapa nchini bado wanatumia teknolojia duni za kilimo kwani takwimu zilizopo zinaonesha kuwa asimia 64 ya wakulima nchini wanatumia jembe la mkono, asilimia 24 wanatumia Wanyama kazi na asilimia 12 tu ndio wanaotumia matrekta

Amesema Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kimefanya tafiti mbalimbali ambazo zina manufaa makubwa kwa wakulima na sekta ya kilimo kwa ujumla hivyo kuwaomba watafiti kuhakikisha tafiti zao zinawafikia wakulima.

Ameongeza kuwa “Sekta ya kilimo bado ndio msingi imara na inachangia asilimia 70 ya ajira kwa Tanzania, asilimia 30 ya bidhaa zinazouzwa nje ya nchi na pia inachangia asilimia 65 ya malighafi zinazohitajika viwandani huku ikichangia asilimia 100 ya chakula kinachotumika hapa nchini”.

Kwa upande wake Makamu wa Mkuu wa Chuo hicho Prof. Raphael Chibunda ameelezea baadhi ya mafanikio yaliyopatikana kupitia chuo hicho ikiwa ni pamoja na kufanya tafiti mbalimbali ambazo zimeleta maendeleo ya wakulima na taifa kwa ujumla, kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi na kufikia 14,581, kupanuka kwa shughuli za chuo.

Awali akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro ambaye amewakilishwa na Mkuu wa Wilaya Bakari Msulwa amekipongeza chuo cha SUA kwa kuienzi kazi kubwa iliyofanywa na Hayati Edward Moringe sokoine, na kutambua mchango wa kiongozi huyo katika kuendeleza sekata ya kilimo

 Akitoa taarifa ya Kumbukizi ya Hayati Edward Sokoine, Naibu Makamu wa Mkuu wa Chuo upande wa Taaluma Prof. Maulid Mwatawala amesema wiki ya kumbukizi ya Hayati sokoine itahusisha Maonesho ya Teknolojia mbalimbali pamoja na kuwepo kwa Mkutano wa Kisayansi utakaofanyika Mei 25 na Mei 26.

“Pia kutakuwa na maonesho ya bidhaa za kilimo, ufugaji na uvuvi, mashindano ya michezo mbalimbali,shughuli za kijamii za upimaji wa afya na mambo mengine mengi tu”, amesema Prof. Mwatawala.

Wiki ya kumbukizi ya 17 ya Hayati Edward Moringe Sokoine kwa mwaka huu imebeba kauli mbiu isemayo“Teknolojia za kilimo Kuzalisha kwa tija na ushindani katika soko la Tanzania kuelekea uchumi wa kati wa juu “.

 

 

Post a Comment

0 Comments