Wataalamu wa masuala ya uchumi nchini, wametaja faida nne ambazo zitaletwa katika uchumi wa nchi kutokana na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Rais Samia Suluhu ikiwamo kupunguza kodi ya mshahara (Paye) kwa wafanyakazi.
Akihutubia katika sherehe za Mei Mosi ambazo zilifanyika kitaifa Jijini Mwanza jana, Rais Suluhu alitangaza kupunguza kodi hiyo kutoka asilimia tisa hadi nane, kitendo ambacho kimetoa faraja kwa wafanyakazi kwani kitaongeza kipato chao.
Katika hotuba yake, mbali na kupunguza Paye, Rais alisema serikali inakwenda kuboresha maslahi ya wafanyakazi, kupandisha vyeo watumishi 85,000 hadi 90,000, kulipa malimbikizo ya mishahara na kuajiri wafanyakazi wapya 40,000.
Kutokana na hatua hizo na nyingine zitakazochukuliwa na Serikali ya awamu ya sita, watalaamu wa uchumi wametaja mambo manne ambayo hatua hizo zitakwenda kuwa na faida ya moja kwa moja kwa wafanyakazi na uchumi wa nchi.
Faida hizo ni pamoja na kiasi ambacho mfanyakazi alikuwa akiondoka nacho nyumbani baada ya kodi (take home) kitaongezeka, mfumuko wa bei utadhibitiwa hautaongezeka, itaongeza mzunguko wa fedha na kuongeza uwezo wa kununua.
Walichokisema wataalamu wa kiuchumi
Akizungumza na gazeti hili jana, Mhadhiri Mwandamizi wa chuo kikuu cha Dar Es Salaam (UDSM), Profesa Deogratius Mushi alisema unapopunguza tozo za kodi kwenye mshahara, inaongeza kiasi cha mwisho cha fedha mfanyakazi anachopata.

0 Comments