Na. James K. Mwanamyoto-Mwanza
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka Viongozi na Watumishi katika Taasisi za Umma kufanya kazi kwa bidii na uadilifu badala ya kuendekeza majungu mahala pa kazi jambo ambalo limekuwa likirudisha nyuma maendeleo ya Utumishi wa Umma na Taifa kwa ujumla.
Mhe. Mchengerwa ameyasema hayo leo, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF Wilayani Magu.
Mhe. Mchengerwa amesisitiza kuwa, Watumishi na Viongozi wasiowajibika hawana nasafi katika utawala wa Serikali ya Awamu ya Sita ambayo imedhamiria kutoa huduma bora kwa wananchi, na kuongeza kuwa atahakikisha Utumishi wa Umma unakuwa na rasilimaliwatu yenye tija.
Mhe. Mchengerwa amefafanua kuwa, Utumishi wa Umma ndio injini ya nchi hii, hivyo Viongozi na Watumishi wa Umma hawana budi kutekeleza majukumu yao kikamilifu ili kuweza kutoa huduma bora kwa wananchi.
Mhe. Mchengerwa amesema kuna baadhi ya Viongozi na Watumishi wenye nyadhifa wamekuwa wakitumia nyadhifa zao kukandamiza watumishi walio chini yao kwa kusikiliza majungu na fitina.
“Tuache kutumia nyadhifa tulizo nazo vibaya hivyo tufanye kazi, na kama kuna mtumishi ambaye amekuwa akitekeleza majukumu yake kikamilifu apewe ushirikiano na andelezwe ili aweze kutoa mchango mkubwa kwa taifa badala ya kujengewa uadui.
Aidha, amewataka Watumishi wa Umma kuwa na utamaduni wa kujiendeleza ili waweze kufika mbali. “Jambo lolote lenye mafanikio ni lazima lianzie mbali, hivyo ni vema kujiendeleza badala ya kubweteka,” Mhe. Mchengerwa ameongeza.
Mhe. Mchengerwa amehitimisha ziara yake ya kuzungumza na Watumishi Wilayani Magu kabla ya kukagua utekelezaji wa shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini katika Kijiji cha Nyashigwe Wilayani Magu.
0 Comments