WAZIRI wa Kilimo Prof. Aldof Mkenda amepiga marufuku kwa jeshi la polisi kukamata wafanyabiashara ya Mahindi wakati wanapeleka bidhaa yao sokoni kwani hali hiyo inakatisha tamaa wakulima.
Prof.Mkenda ametoa Kauli wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua na kujionea Mashamba ya Kilimo cha mkataba wa zao la mtama wilayani Kongwa.
Waziri Mkenda amesema kuwa anatarajia kuzungumza na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) kuhakikisha Jeshi hilo linaachana na tabia ya kukimbizana na wafanyabiashara hao wakati wakipeleka biashara zao sokoni.
“Kuna changamoto kubwa ya masoko inayowakabili wafanyabiashara wa mahindi nchini, wafanya biashara hao wanauhuru wa kufanya biashara eneo lolote nchini kwa kuwa wanakuwa wakitafuta masoko, hivyo kuwazuia na kuwanyang’anya mazao yao wakati wakipeleka sokoni ni kuwavunja moyo na kuwakatisha tamaa,”amesema Prof.Mkenda.
Hata hivyo Prof. Mkenda amewataka askari wa Jeshi la Polisi nchini kuacha tabia hiyo ya kuwanyanyasa na kuwasumbua wakulima na wafanyabiashara wa zao hilo ambao wanakuwa wakipambana kujikwamua na umaskini na kuchangia pato la taifa.
“Hiki kitu kwa kweli sio kizuri hawa ni watanzania ambao wanatafuta masoko ya zao hilo ni vema wakaachiwa ili kuendelea na biashara hiyo”amesema Prof. Mkenda
0 Comments