Na Gerald Lwomile
Morogoro
Serikali imekipongeza Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)
kwa kuanza kuchukua hatua za kusaidia uwepo wa malisho ya uhakika kwa wakulima
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Mashauri Ndaki akizungumza na wadau wa malisho
Pongezi hizo zimetolewa April 21, 2021 mkoani Morogoro na
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Mashauri Ndaki wakati akifungua
shughuli za Siku ya Malisho iliyoandaliwa na Chama cha Nyanda za Malisho
Tanzania
Amesema SUA ambacho kupitia Mradi wa Innove Afrika umeanza
kuchukua hatua ya uzalishaji malisho nchini hatua ambayo itasaidia sana
kupunguza uhaba na migogoro kati ya watumiaji rasilimali ardhi na kuongeza upatikanaji wa malisho bora kwa wanyama.
Ameongeza kuwa ni vyema wafugaji kulinda rasilimali za nyanda
za malisho na kuziboresha kwa kupanda malisho aina mbalimbali.
Mhe. Ndaki ameahidi
kuwatembelea wazalishaji wa malisho aina ya Brachiaria huko Rungwe mkoani Mbeya na kuwataka wataalamu wa halmashauri ya Rungwe walioambatana na wazalishaji hao kuongeza idadi ya wazalishaji wa malisho
hayo.
Wakati huo huo Serikali imekiri kuwepo kwa tatizo kubwa la
malisho nchini na kusema kuwa kama hatua za dharura hazitachukuliwa nchi iko
kwenye wakati mgumu wa kuhakikisha kunakuwa na ufugaji endelevu nchini
Mhe. Ndaki amesema kuwa Tanzania ina namba kubwa ya mifugo
ikiwa katika nafasi ya pili barani Afrika na kutokana na hali hiyo nchi hii
ingekuwa imepiga hatua kubwa za kimaendeleo kwa mifugo iliyopo lakini kutokana
na watu kushindwa kufuga kisasa na kibiashara mifugo imekuwa na pato dogo kwa
mfugaji na Taifa kwa ujumla
Waziri huyo wa Mifugo na Uvuvi amesema pamoja na kuwepo kwa
mifugo hiyo pia kumekuwa na tatizo la maeneo ya kulishia mifugo na wafugaji
kushindwa kulinda maeneo ambayo yametengwa kwa ajili yao na kuepuka kuingia
katika maeneo ambayo si yao ili kuepuka migogoro ya wakulima na wafugaji
“Kwa sababu mfugaji anahangaika kuangalia ni kwa namna gani
atalisha huo mfugo wake, huyo anayefugwa naye anahangaika tu kwa sababu hana
malisho ya kutosha kwa hiyo kila mmoja anakonda tu, kila mmoja anamuonea huruma
mwenzake” amesema Mhe. Ndaki
Awali akimkaribisha Waziri wa Mifugo na Uvuvi ili afungue siku
hiyo Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare amesema viongozi wengi katika
maeneo mbalimbali wasio waaminifu wamekuwa hawana taratibu nzuri za utoaji wa
ardhi jambo ambalo lilisababisha kuwepo kwa migogoro baina ya wakulima na
wafugaji
“Na mapigano haya yanatokana na kutoheshimiana na uongozi
mbovu wa viongozi wetu kule vijijini, kumekuwa na utaratibu wa kutoheshimu au
kutopanga mipango bora ya matumizi katika vijiji vyetu, watu wanaingia katika
maeneo mbalimbali ya mkoa wa Morogoro kwa fujo sana jambo linalosababisha
vurugu baina ya wakulima na wafugaji”, amesema Sanare
0 Comments